skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Mbunge wa Kasulu mjini Profesa Joyce Ndalichako amewashukuru wananchi wa jimbo lake, serikali na chama cha mapinduzi (CCM) kwa kuendelea kumpa heshima ya pekee wakati wa mazishi ya mama yake mzazi Bi. Mary Ivo Ndalichako ambaye amefariki jijini Dar es Salaam na kuzikwa katika makaburi ya Mtakatifu Francis Exavery parokia ya Kasulu

Akitoa shukurani wakati wa Misa ya kumuombea marehemu mama yake katika kanisa Katoliki kigango ya mtakatifu Paulo Mtume Mwilamvya mjini Kasulu, kabla ya mazishi, Profesa Ndalichako ameweka bayana hisia zake za kuungwa mkono na maelfu ya wananchi, viongozi wa vyama na serikali katika kumuuguza na hatimaye mazishi ya mama yake.

Nimethibitisha mwenyewe kuwa wana Kasulu mnanipenda sana, wakati wa uchaguzi mlinipa kura nyingi sana za Ubunge na leo mmeonesha dhahiri kuwa mnanithamini, si tu katika siasa bali hata katika jambo hili mmekuwa nami, ninawashukuru sana na ninaliona hili kuwa ni deni kubwa linalonitaka nizidi kuwatumikia na ninaahidi kuwa nitatumia uwezo wangu kushirikiana nanyi kuleta maendeleo” Alisisitiza Ndalichako wakati akitoa shukurani Kanisani.

Profesa Ndalichako pamoja na ndugu zake wakiwa katika kanisa la Mwilamvya mjini Kasulu

Wakati huo huo Mwakilishi wa serikali Mheshimiwa George Simbachawene ambaye ni waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu na Bunge aliyeleta saalaam za serikali akiwemo Samia Suluhu Hassan Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dr. Philip Mpango Makamu wa Rais na Kassim Majaliwa waziri Mkuu, katika mazishi ya mama wa Mbunge huyo ametoa pole kwa familia na kukiri kuwa maisha ya marehemu Mary Ndalichako yameacha alama mhimu kwa familia, kwa kanisa na taifa kwa ujumla

George Simbachawene Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge akitoa salaamm za serikali wakati wa ibada ya kumuombea mama mzazi wa profesa Joyce Ndalichako, mama Mary Ivo Ndalichako mjini Kasulu

Naye Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Kigoma Mhashamu askofu Joseph Mlolwa ametoa wito kwa waumini wa kanisa hilo kuiga maisha ya sala na upendo kama alivyofanya marehemu Mary wakati wa uhaii wake huku akitaja kuwa kumcha Mungu ni sehemu ya kuandaa maisha mapya baada ya kifo

Mhashamu Baba Askofu Joseph Mlola, askofu wa jimbo la Kigoma akitoa neno wakati wa ibada ya kumuaga Mama Mary Ivo Ndalichako katika Kigango cha Mwilamvya Kasulu.

Wakati huo huo mtoto wa marehemu Mary Ndalichako, Padre Dr. Evance Ndalichako ambaye ni Mhadhiri wa chuo kikuu cha RUAHA (RUCO) kinachomilikiwa na kanisa katoliki, ameongoza ibada ya mazishi ya mama yake huku akifurahi kuwa malezi waliyopewa yeye na ndugu zake ni zawadi tosha kwa mungu.

Padre Dr. Evance Ndalichako (mwenye vazi la zambarau) akiongoza Ibada ya mazishi ya mama yake mzazi Mary Ivoo Ndalichako

Mama Mary Ivo Ndalichako amefariki na kuzikwa akiwa na umri wa miaka 82, na alitumikia utumishi wa umma katika kada ya ualimu kwa miaka takribani 40 pamoja na miaka kadhaa ya usaidizi katika shule ya msingi na malezii ya Calmel inayomilikiwa na maststa parokia ya Katubuka.

Ibada ya kumuombea Marehemu Mary Ivo Ndalichako katika kanisa la mtakatifu Paulo Mwilamvya Kasulu

Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe,

Raha ya milele Umpe Ee Bwana na Mwanga wa Milele umwangazie, aumzike kwa Amani …..AMINA

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma