skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amekagua maandalizi ya sherehe za Mei Mosi na kueleza ameridhishwa na hatua zilizofikiwa.

Amesema hayo Aprili 20, 2023 baada ya kupokea taarifa ya kamati ya maandalizi walipokutana kwa lengo la kujadili na kupanga mipango mbalimbali kuelekea kilele cha sherehe hizo zinazotarajiwa kuadhimishwa katika uwanja wa Jamhuri, Mkoani Morogoro.

Aidha, Waziri Ndalichako amepongeza kamati ya mkoa kwa kushirikiana na ofisi yake pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ili kufanikisha sherehe hiyo.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri, hakika hatua iliyofikiwa katika maandalizi inaridhisha,” amesema

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mei Mosi alipokutana nao katika ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe, Mkoani Morogoro. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi

“Nipongeze Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kwa namna wanavyoratibu shughuli hii na tunawaunga mkono kwa kuwa tunatambua umuhimu wa wafanyakazi katika kutekeleza malengo ya Serikali,”

Sambamba na hayo amehamasisha wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 1 Mei, 2021.

Prof. Ndalichako pia ametumia fursa hiyo kushukuru wadhamini na wadau mbalimbali kwa michango yao ambayo itasaidia kufanikisha shughuli hiyo. Vilevile amewataka wanakamati kuendelea kusimamia shughuli zinazofanyika uwanjani hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa akitoa taarifa ya hatua za maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mei Mosi wakati wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe, Mkoani Morogoro.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa amesema kuwa mkoa huo umejipanga vizuri katika kufanikisha sherehe hiyo muhimu kwa kuzingatia mambo matano ya msingi ikiwemo kuratibu suala la rasilimali fedha za maandalizi, kuandaa uwanja wenye hadhi, kuhamasisha wananchi kushiriki kwa shamrashamra kuelekea siku hiyo na kutangaza maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi.

Maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi 2023 yataadhimishwa kitaifa katika mkoa wa Morogoro, yakiwa na kauli mbiu isemayo “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa.”

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma