skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako siku chache baada ya kukabidhiwa ofisi ameanza kwa kuamsha ari ya jamii, wadau na mashirika ya maendeleo kuungana na serikali kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo mapema jana katika hafla ya kukabidhi Viti Mwendo na Kadi za Bima ya Afya kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Boabab Ballroom hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha ambapo amehimiza wadau kuwajengea uwezo na kuwezesha Watu wenye Ulemavu kupata vifaa saidizi na nyenzo bora za kujimudu kijamii na kiuchumi  

Alisema kuwa Watu Wenye Ulemavu wanahitaji vifaa saidizi ili waweze kumudu mazingira yanayowazunguka, nyenzo hizo za kujimudu ni pamoja na viti mwendo, shime, sikio, fimbo nyeupe, ubao wa kuandikia maandishi ya nukta nundu, kofia, miwani, magongo ya kutembelea na vingine vingi, hivyo kutokana na umuhimu wa vifaa hivi upatikanaji wake ni vyema wadau wakashirikiana na Serikali katika kuwezesha Watu wenye Ulemavu kupata vifaa saidizi na nyenzo bora za kujimudu.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo mkubwa kwenye kuwasaidia Watu Wenye Ulemavu ikiwemo huduma za kijamii kuboresha ili kutoa fursa Watu Wenye Ulemavu kuzipata kwa urahisi,” alieleza Waziri Ndalichako

“Mmeshuhudia namna Serikali imekuwa ikikaribisha na kupokea misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama hii leo walivyofanya wadau kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mrisho Gambo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini katika kusaidia Watu Wenye Ulemavu,” alisema

Alieleza kuwa, Serikali katika kutambua uhitaji mkubwa wa vifaa saidizi kwa Watu Wenye Ulemavu Serikali imeweka jitihada ya kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana kwa wingi zaidi hapa nchini kwa kuanza kuzalisha vifaa hivyo kupitia Shirika la Maendeleo la Viwanda vidogodogo (SIDO).  

Pia, Serikali imeondoa kodi kwenye malighafi zote za kutengenezea vifaa vya Watu Wenye Ulemavu hapa nchini ili kuongeza uingizaji wa vifaa hivyo nchini na kuhakikisha vinapatikana kwa gharama nafuu.

Vile vile, alisema kuwa Serikali imeendelea kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo Watu Wenye Ulemavu katika kutafuta fursa na huduma za kijamii ikiwemo Elimu, Afya na Ajira.

Imeandaliwa na mwandishi wetu, Wizara ya Kazi

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma