skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki,Simiyu 

Wakulima mkoani Simiyu wanatarajia kunufaika na  kuongeza uzalishaji wa pamba  mara baada ya kupatikana kwa ndege zisizikuwa na rubani  (drones) kwaajili ya kunyunyizia dawa za kuulia wadudu waharibifu wa pamba.

Uwepo wa teknolojia hiyo ya  kisasa kwenye upuliziaji wa dawa za kuulia wadudu waharibifu wa pamba unatajwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo msimu ujao kutoka asilimia 60 ya sasa hadi kufikia asilimia 80.

 Akiwa kwenye maonesho ya kanda ya ziwa mashariki inayohusisha mikoa ya Mara,Shinyanga na Simiyu wenyeji ambayo kikanda yamefanyika kwenye viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi   mkaguzi wa pamba kutoka bodi ya pamba Said Itaso amesema kwanza wataanza kuwatambua wakulima wakubwa ambao wanalima kuanzia hekari 5 na wakishawatambua linafuata zoezi la upuliziaji na huduma hiyo itakuwa ikitolewa bure.

“Sisi tupo tayari kuwahudumia muda wote kwa teknolojia hii mpya kwahiyo walime tu mashamba ya kutosha hawatapata shida tena upuliziaji kwa kubeba pamp zile za mgongoni huduma hii ni bure” amesema  Itaso

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda akizungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari kuhusu mkakati wa kilimo cha pamba mkoani Simiyu

Akiwa kwenye banda la bodi ya pamba lililopo kwenye  maonesho hayo mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda  amesema ujio wa teknolojia hiyo (drones) ni mkombozi mkubwa kwenye uzalishaji wa pamba mkoani humo.

“Kikubwa sisi kuongeza uzalishaji na bodi ya pamba watakuwa wanatoa huduma hizi bure ili kurahisisha kazi na sisi kazi yetu itakuwa ni kulima nichukue nafasi hii kuishukuru bodi ya pamba nishukuru wizara kwa kazi nzuri ambayo inaenda kufanyika na kuleta mapinduzi katika mkoa wetu, mwaka huu tumepanga kuvuna tani laki 250 na laki tatu kwahiyo  kwa teknolojia hii, mwakani msimu wa 2023/24 tunaweza kuzalisha tani laki tano hiyo ndio adhima yetu mkoa wa Simiyu ili tufikishe  asilimia 80 ya pamba yote  itoke katika mkoa wa Simiyu na  tunaweza”Dkt Nawanda

Nao baadhi ya wakulima wamesema  awali walianza kupunguza hekari za kilimo hicho kutokana na gharama za uzalishaji ikiwemo changamoto ya wadudu lakini kwa kupatikana kwa teknolojia hiyo ya unyunyiziaji wameahidi kuongeza idadi ya hekari kutokana na uwepo wa uhakika wa upuliziaji wa dawa za kuulia wadudu waharibifu wa zao hilo kwa kutumia drones.

“Nilikuwa nalima heka kuanzia kumi na kuendelea lakini kulingana na wadudu wanavyotushambulia niliamua kukacha kilimo lile zao nipunguze kabisa lakini kwakuwa nimekuta hii teknolojia imeshatoka hapo nitajitahidi hata heka 20 nalima maeneo ninayo” Dotto Mhonzu,Mkulima wa pamba 

“Ilikifikia wakati nilikuwa nimekata tamaa kabisa kuendelea na zao la pamba lakini kupitia hii teknolojia niliyoiona hapa naamini mwaka huu nitalima zao la pamba, kunyunyizia hekari moja unanyunyizia kontena nne mpaka tano sasa ukiwa hekari  tano unapata kontena nyingi sana kwa hiyo ilikuwa ni adhabu kubwa sana kwa mkulima mpaka kumaliza eneo lote ilikuwa inanichukua siku nne mpaka tano kwa ujumla ilikuwa ni adhabu kubwa” Maduhu Nyanda,Mkulima wa pamba 

Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa inayolima pamba ambapo nusu ya pamba yote inazalishwa mkoani humo, na tayari mkoa huo umepokea drones saba na drone moja unauwezo wa kunyunyizia hekari moja ndani ya dk 15.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma