skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Shirika lisilo la kiserikali la OHIDE linalomiliki kituo cha Radio BUHA FM limewatunuku vyeti waandishi wa habari saba kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, walioshiriki mafunzo ya uandishi wa habari unaozingatia maslahi ya jamii na kuleta matokeo chanya kwa umma.

Mshauri wa shirika la OHIDE Bw. Optatus Likwelile ametoa vyeti hivyo katika hafala fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Serengeti Park mjini Kasulu Mkoani Kigoma, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wadau wa habari akiwemo Katibu Mtendaji wa shirika la OHIDE Silles Malli na wanachama wengine wa OHIDE.

Akizungumza baada ya zoezi la ugawaji wa vyeti Bw. Likwelile amewaasa waandishi wa habari hao kuitumia vyema elimu waliyoipata kwa muda wa siku saba kwa maslahi ya jamii na kutanguliza uzalendo katika kila kazi wanazo zifanya.

Mussa Mkilanya (kulia), mwanahabari kutoka Dar es Salaam akipokea cheti kutoka kwa Mgeni rasmi

“Elimu hii mliyoipata muende mkaitumie vyema mkaitumike jamii ili iweze kupata haki yake ya masingi kisheria ya kupata habari, zingatieni uandishi wenye kufuata misingi ya sheria na kuepuka kuleta uchochozi” amesema Likwelile.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa shirika la OHIDE Silles Malli, amesema umefika wakati waandishi wa habari waache kuandika habari kimazoea, na badala yake waandike habari za kisasa zinazo jibu maswali ya wananchi.

“Nawapongeza sana kwa kushiriki mafunzo haya, mkayatumie vyema, mkaitumikie jamii hakikisheni mnaacha uandishi wa habari wa mazoea andikeni habari kulingana na wakati, habari zijibu maswali ya wananchi na kutatua changamoto zao,” amesema Silles Malli.

Bi. Silesi Malli, Katibu mtendaji wa Shirika la OHIDE akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo kwa wanahabari

Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Prosper Kwigize, amesema elimu ya uandishi na utangazaji ni elimu mtambuka na inahitaji umakini na weledi na ubunifu wa hali ya juu ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia, mabadiliko ya kibinadamu na kimazingira.

Amebainisha kuwa vyombo vingi vya Habari vinafanya makosa mengi katika mpangilio wa Habari na vipindi kutokana na kujifikiria vyenyewe badala ya kushirikiasha jamii kubuni maudhui ambayo yanagusa maslahi ya msikilizaji na kuleta matokeo chanya au mageuzi katika jamii husika.

Kuhusu Tabia ya vituo vingi vya Radio kuwa kumbi za muziki, Kwigize amebainisha kuwa inatokana na watangazaji kutokuwa na ujuzi wa kufikiri kuhusu nafasi ya muziki katika kuelimisha na kuhabarisha jamii na hivyo wao wanasalia na dhana moja tu ya kuburudisha.

“Muziki ni kipengere mhimu katika utangazaji, lakini kikitumika vibaya hakutakuwa na utofauti kati ya chombo cha Habari na ukumbi wa muziki (DISCO) na hali hii inapelekea radio nyingi kukosa wasikilizaji wa kutosha na hivyo kukosa matangazo ya kibiashara.

Amesisitiza kuwa siku hizi kila mwananchi wanaweza kuwa mtangazaji wa DJ, na akaamua wimbo au muziki gani ausikilize, lakini kitakachokosa kwake ni taarifa sahihi kuhusu wimbo, mtunzi na mahala ulipotungwa sambamba na sababu za kutungwa kwa wimbo au muziki husika.

Kwigize amehimiza kuwa wajibu wa chombo cha Habari ni kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi ambazo zikitumika vizuri zitaborehs Maisha ya msikilizaji na kuteta tija kwa jamii.

Ananias Khalula (kulia) kutoka mkoani Kagera akipokea cheti baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya kimkakati

Wakitoa neno la shukrani waandishi hao wamesema, wanalishukuru shirika la OHIDE kwa kuwapatia mafunzo ambayo yamewabadilisha kifikra kutoka kwenye uandishi wa habari wa kimazoea ambao unatumiwa na waandishi wengi hapa nchini.

Waandishi walioshiriki mafunzo hayo ni Mussa Mkilanya kutoka mkoa wa Dar es salaam, Ananias Johakim Khalula na Joel Daud kutoka mkoa wa Kagera, Matinde Nestory kutoka mkoa wa Mwanza, Kitungwa Evaresti Edison na Nurdni Ayubu kutoka mkoa wa Kigoma.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma