skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu

Asasi ya uwekezaji katika Utu na Maendeleo OHIDE Tanzania yenye makao maku wilayani Kasulu, leo imetoa msaada wa mashine ya kutatua changamoto ya upumuaji kwa watoto wachanga wanaozaliwa na matatizo ya kiafya katika hospitali ya rufaa ya Kabanga wilayani Kasulu

Utoaji wa msaada huo wa kifaa tiba umefanyika katika wodi ya wazazi na watoto wachanga kama sehrmu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka juni 16 kama kumbukumbu ya mauaji ya watoto wa Afrika Kusini yaliyofanya na askari wa serikali ya kibaguzi mwaka 1976.

Akitoa taarifa juu ya maadhimisho ya sherehe hiyo pamoja na hisani ya kifaa tiba, katibu mtendaji wa shirika la OHIDE Bi. Silesi Malli ameeleza kuwa asasi hiyo imeungana na asasi ya Wanawake laki moja, kituo cha habari cha Buha FM, BUha TV Online na kambuni ya Ulinzi ya wanajeshi wastaafu MUWAWATA kununua mashine hiyo ambayo itaokoa maisha ya watoto ambao huwa katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na changamoto ya kupumua wakati wa kuzaliwa.

Bi. Silesi Malli, katibu mtendaji wa shirika la OHIDE Tanzania na Mhamasishaji wa asasi ya wanawake 100,000 mkoani Kigoma

Awali Katibu mtendaji wa asasi ya wanawake laki moja ya mkoani Kigoma Bi. Sakina Kabeza alibainisha kuwa mashirika hayo kwa pamoja yanatambua kuwa mtoto huanzia mimba inapotungwa, na siku mama mjamzito anapojifungua na kwamba ulinzi thabiti wa mtoto wa Afrika lazima uendane na kujali afya ya mama na mtoto akiwa tumboni na anapozaliwa

hata hivyo Kabeza ametahadharisha kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanyika kabla na baada ya kuzaliwa ikiwemo utoaji wa mimba, kutupa au kutelekeza watoto, kuingiliwa kinyume na maumbile, ulawiti, ushoga na mapenzi ya jinsia moja.

Ametoa Wito kwa watoa huduma za afya hususani wauguzi, madaktari na wataalamu wa maabara kutoa taarifa za haraka kwa vyombo vya dola na idara ya ustawi wa jamii pindi wanapopokea mgonjwa hasa mtoto aliyefanyiwa ukatili wa aina yoyote.

Aidha, Kabeza ameonya juu ya matumizi ya zana za kidijitali hususani simu na runinga kwa watoto akitaja kuwa kwa sasa vinatumika vbaya kwa kueneza maudhui yasiyofaa na yanayohamasisha udhalilishaji wa watoto ikiwemo filamu za ngono, mauaji na mafunzo ya ndoa za jinsia moja.

Daktari Ogendo Simon akitoa shukurani kwa mashirika ya OHIDE, MUWAWATA na Wanawake laki moja kwa msaada wa kifaa cha tiba kwa watoto wachanga

Akitoa shukurani, kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Daktari Ogendo Simon amebainisha kuwa taasisi za afya pamoja na shughuli za tiba wanajihusisha pia na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hususani dhidi ya watoto kuanzia malezi ya mimba na wanapozaliwa, hivyo kifaa walichopokea kitasaidia kulinda na kupigania uhai wa mtoto

Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii katoka hospitali hiyo Bw. Laurent Kaje amebainisha kuwa hospitali hiyo ni moja na vituo ambavyo vikuwa vikiwapokea watoto walioathiriwa au kutendewa ukatili na kwamba karibu watoto 5 hadi 7 kati ya 10 wanaofikishwa katika hospitali hiyo hukutwa wamefanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kutopewa huduama stahiki za kijamii, kutelekezwa nakadharika,

Picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa haki na ulinzi wa mtoto wilayani Kasulu wa kwanza kushoto ni afisa ustawi wa hospitali ya Rufaa Kabanga Bw. Laurent Kaje

Bw. Kaje amesisitiza kuwa jamii hasa wanawake wameingia katika kutenda vitendo vya ukatili zaidi kutokana na mashinikizo ya kijamii na kidijitali na kwamba wengi wanatoa mimba au kutamani kutonyonyesha watoto ili wasalie na muonekano wao wa ubinti jambo ambalo huchochea ukatili kwa watoto.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka June 16 kama kumbukumbu ya mateso na mauaji dhisi ya watoto yaliyotekelezwa na askari polisi makaburu wa Afrika kusini mwaka 1976.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma