skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Nduta Kibondo

Wakimbizi wa Burundi wanaoishi katika kambi ya Nduta na Nyarugusu magharibi mwa Tanzania wameitaka serikali ya Burundi kuzungumza na kufanya maridhiano makundi ya waasi wa nchi yao ili kupata suluhu ya kisiasa na kutoa mwanya kwao kurejea nchini mwao.

Kauli hiyo imetolewa kambini humo mbele ya Naibu waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Bw. Nimbona Celestin wakati akiwahutubia wakimbizi na kuwahimiza kurejea nchini Burundi

Wakimbizi hao wamewataja Leonard Nyangoma na Niyombare Godfrey wanaotuhumiwa kushiriki jaribio la mapinduzi ya hayati Pierre Nkurunziza mwaka 2015 kuwa ni sababu ya kukimbia kwao na kwamba kuendelea kuishi uhamishoni kwa wanasiasa hao wanaotuhimiwa kwa vitendo vya uasi ni kikwazo cha kurejea kwa wakimbizi walio wengi.

Naibu waziri wa Mambo ya ndani Burundi Nibona Celestin akifafanua jambo kuhusu hali ya amanni nchini Burundi

Ntakirutimana Alexandre ni mmoja katii ya wakimbizi wa Burundi aliyekimbia mwaka 2015 kufuatia kuibuka kwa maandamano makubwa yaliyofuatia jaribio la mapinduzi ya serikali ya hayati Nkurunziza, yeye pamoja na wengine wengi wanataja kuwa kitendo cha Nyangoma na Niyombare kuendelea kuishi uhamishoni kinawatia shaka juu ya uendelevu wa amani iliyopo.

Hata hivyo Naibu waziri Nimbona Celestin ametaja kuwa Burundi Serikali ya Burundi iko imara kuzuia aina yoyote ya chokochoko kutoka ndani au nje ya nchi hiyo na kwamba wakimbizi hawapaswi kuwa na hofu yoyote kwakuwa warundi zaidi ya milioni 12 wako nchini mwao na wanaishi kwa amani.

Kuhusu hoja za hakikisho la kurejea kwa Nyangoma na Niyombare, NImbona amekiri kuwa kitendo cha wakimbizi hao kuleta madai ya aina hiyo kinaifanya serikali ya Burundi kuamini kuwa katika kambi za wakimbizi wamo wafuasi wa viongozi hao waliokimbia na anawatoa hofu wakimbizi kuwa hawana sababu ya kutorejea kwa kisingizio cha Niyombare na Nyangoma ambao wana maisha mazuri kuliko wao uhamishoni.

Nimbona ametaja kuwa warundi kadhaa walioshabikia jaribio la mapinduzi na kukimbilia Rwanda, Tanzania na DRC walisharejea na hakuna serikali iliwasemehe, na kwamba Nyangoma na Niyombare watatakiwa kujibu mashtaka dhidi yao kwa mujibu wa sheria za Burundi na za kimataifa.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma