Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka…
Na Anita Balingilaki
Serikali kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB) imenunua na kusambaza jumla ya ndege zisizokuwa na rubani 20 kwa ajili ya kunyunyizia dawa za kuua wadudu kwa wakulima wenye mashamba makubwa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mhandisi Kisinza Ndimu kutoka Bodi ya Pamba wakati wa uzinduzi wa zoezi la unyunyiziaji wa dawa kwa kutumia ndege hizo ambao umefanyika kata ya Budalabujiga wilayani Itilima mkoani hapa na zina uwezo wa hekari 15 hadi 20 kwa saa.
Ndege hizo zimesambazwa kwenye baadhi ya wilaya zinazolima zao la pamba nchini lengo likiwa kuwawezesha wakulima kukabiliana na changamoto ya wadudu waharibifu wa zao hilo.
Kati ya ndege hizo, saba zimepelekwa mkoani Simiyu kwa ajili ya kunyunyizia mashamba makubwa ya pamba ambapo mkulima atanyunyiziwa shamba lake pasipo gharama yoyote.
Mhandisi Ndimu amesema wamefanya majaribio katika wilaya ya Itilima kwa kutumia ndege hizo ambazo zitatumika kupulizia mashamba makubwa ya Pamba.
” Bodi ya pamba tumekuwa tukitoa pembejeo kwa wakulima, mbegu, viuatilifu pamoja ni pampu za kupulizia ambazo hubebwa mgongoni kwa hali ilivyo wakulima wengi wana mashamba makubwa, tumeona ili kurahisisha kazi tuwaletee ndege zisizo na rubani (drone)” amesema Mhandisi Ndimu.

Aidha amesema mashine hizo zitasaidia wakulima wa pamba kutumia muda mchache wakati wa kupulizia,huku akiongeza kuwa pampu za kawaida mkulima alikuwa anatumia muda mwingi kupulizia na kuchoka hasa akiwa na shamba kubwa.
Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Itilima Said Itaso amesema awali walikuwa wanakutana na changamoto ya upuliziaji kwa wakulima wakubwa wa pamba ambao walikuwa wanahitaji teknolojia ili kurahisisha zoezi la upuliziaji wa mashamba yao.
Itaso amesema changamoto kubwa aliyokuwa akikutana nayo kwa wakulima hususan wenye mashamba makubwa kuanzia ekari 10 hadi 50 wengi walitumia siku nyingi kukamilisha kisha zoezi hilo huku akiongeza kuwa ujio wa mashine hizo imekuja kwa muda mwafaka.
Nao baadhi ya wakulima kutoka Budalabujiga wakaipongeza serikali huku wakisema kuwa ujio wa ndege hizo utawawezesha kuongeza tija kwenye uzalishaji wa pamba hatua itakayowaongezea kipato cha familia zao.
Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa inayolima pamba kwa wingi huku ikitajwa kuzalisha nusu ya pamba yote nchini.