skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki ,Simiyu

Mkuu wa mkoa wa simiyu Dkt Yahaya Nawanda amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe na fedha hizo zitumike kama ilivyopangwa.

Dkt Nawanda amesema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya lishe na mipango ya awali ya bajeti 2023/24 kilichofanyika wilayani Bariadi mkoani Simiyu

Wadau wa Lishe mkoa wa Simuyu wakisikiliza kwa umakini maelekezo ya mkuu wa mkoa wa Simiyu katika kikao cha pamoja cha viongozi na wadau wakiwemo wakurugenzi na wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Simiyu. Picha na. Anita Balingilaki

Ameeleza kuwa suala la lishe linapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa na fedha zinazotengwa kutekeleza afua za lishe zitumike ipasavyo, huku akionya kuhusu ubadhilifu katika mipango ya maendeleo.

“Wakurugenzi niwatake sasa afua zote zile na suala la lishe linakuwa ni suala muhimu sana kwenu… likija kwenye meza, mhakikishe mnatenga fedha na zinatumika ipasavyo kutokana na afua inavyotaka, hilo ni jambo muhimu sana na haya yote ni maagizo ambayo wakati mwingine tutakapokuja kuyazungumza yatakuwa kama maazimio yetu ya kikao, kwahiyo fedha zitengwe lakini pia mkishatenga hiyo shilingi elfu moja ikatumike vizuri kutokana na zile afua.” amesema Dkt. Nawanda.

Aidha Dkt Nawanda amesisitiza suala la wanafunzi wa shule zilizopo mkoani hapo kupatiwa uji shuleni na kufikia mwakani wapewe uji na chakula.

“Ajenda ya kuhakikisha watoto wanakula chakula mwakani.. tumekubaliana watoto wetu katika shule zote zaidi ya 700..shule za msingi 700 nilizonazo mimi hapa katika mkoa wa Simiyu zote nataka zianze kupata chakula asubuhi na mchana, tukianza na watoto wa awali wapate uji na shule za sekondari pia, na tukienda mbele zaidi hata chakula cha mchana tuanze kutoa, tukifanya hivyo basi tutaimarisha afya za watoto na mwisho wa siku afua zitakuwa tumezitekeleza kwa asilimia 100 na mkoa wetu tutang’ara, Simiyu hatuna jambo dogo kila jambo sisi ni jambo kubwa.” amesema Dkt Nawanda.

Kutoka kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Maswa Mh. Aswege Kaminyoge (mwenye suti) na Mh. Lupakisyo Kapange (kulia) mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wakisikiliza kwa umakini maagizo ya Dkt Nawanda. Picha na Anita Balingilaki

Kwa upande wake afisa lishe wa mkoa wa Simiyu Dkt Chacha Magige amesema kuwa karibia asilimia 99 ya watoto mkoani humo wananyonyeshwa maziwa ya mama, huku akitaja kuwepo kwa changamoto ya matumizi ya chumvi isiyo na madini joto.

“Bahati nzuri tuliyonayo kama mkoa ni kwamba angalau watoto karibia asilimia 99 wananyonya maziwa ya mama ingawaje hawafuati utaratibu ambao unakubalika, lakini changamoto tuliyonayo ni matumizi ya chumvi iliyotiwa madini joto, kwa takwimu za mwaka 2018 ni asilimia 23 ndizo zinatumia chumvi yenye madini joto, na hii inatokana na kwamba sisi mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa ambayo inazalisha chumvi kwahiyo chumvi hiyo tunayozalisha ni rahisi mtu anaweza kuchukua kiasi kikubwa kwa gharama ndogo halafu akahifadhi akawa anatumia hata kwa mwaka mzima.” amesema Dkt Magige.

Hivi karibuni Rais wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa taifa kuzingatia masuala ya Lishe akitaja kuwa jamii mbalimbali zinakabiliwa na matatizo ya kiafya yanayotokana na lishe duni, akiwataka wakuu wa mikoa kusimamia mipango ya Lishe na elimu kwa umma kuhusu afya ya jamii.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma