skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka vijana wasiogope kukopa ili kupata fedha za mitaji ya kibiashara lakini pia akawasisitiza wawe tayari kurejesha mikopo hiyo.

“Vijana wetu msiogope kukopa ili kupata mitaji. Bila kukopa huwezi kupata maendeleo. Eneo muhimu ni kupata taasisi za fedha kama CRDB lakini kikubwa zaidi ni kuwa tayari kulipa. Dawa ya kukopa ni kulipa,” amesema.

Ametoa wito huo leo wakati akizungumza na washiriki  waliohudhuria semina ya uwekezaji na ufunguzi rasmi wa dirisha la kupokea maombi ya ushiriki wa programu ya iMBEJU ya Benki ya CRDB uliofanyika kwenye ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam. 

iMBEJU ni programu maalumu ya CRDB ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake wajasiriamali ambayo ilizinduliwa Oktoba, 2022 katika Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika Zanzibar.

Waziri Mkuu amewataka vijana na wanawake wajasiriamali watakaoshiriki programu hiyo waitumie fursa hiyo ipasavyo hasa ikizingatiwa kuwa watawezeshwa kupata elimu ya biashara, stadi za biashara na pia watawezeshwa kimitaji. Benki ya CRDB imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Kamisheni ya Tehama (ICT-C) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika kuinua vipaji kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.

Waziri mkuu akizungumza na vijana wajasiriamali

Akizungumzia baadhi ya miradi ya ubunifu ambayo aliiona kwenye maonesho, Waziri Mkuu amesema kuna vijana wamebuni mfumo wa kuzuia msongamano kwenye taa za barabarani na kuruhusu magari ya wagonjwa yapite haraka endapo kuna dharura imetokea.

“Wizara ya Ujenzi waone njia ya kuwawezesha vijana hawa ili waanze pilot project pale kwenye taa za UWT, FIRE na Muhimbili. Na kama siyo hapo, watafutiwe barabara nyingine yenye msongamano ili waweke mfumo wao na waoneshe ubunifu wao na pia sisi tupate suluhisho,” amesema.

Amesema Serikali imeendelea kutumia mifuko ya kukopesha vijana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na mitaji iliyokuwa ikikwamishwa na uwepo wa masharti magumu kutoka kwa taasisi za fedha ikiwemo mabenki. “Kwa mfano, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.88 imetolewa kwa miradi 85 ya vijana.”

Fuatilia mjadala huu kupitia ukurasa wetu wa twitter wa Buha FM Radio na uwe huru kutoa maoni ili tusaidie vijana kutoogopa kukopa

Akizungumzia hatua za kisera za kukabiliana na changamoto ya ajira, Waziri Mkuu amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kuita wawekezaji na kutoa fursa ya elimu kwa kila Mtanzania.

“Serikali imeendelea kuimarisha, kukuza na kusimamia ubora wa elimu inayotelewa nchini ili kuwapatia wananchi wake nyenzo stahiki za kupambana na umaskini. Miongoni mwa miradi ya kuboresha sekta ya elimu ni mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) ambapo kupitia mradi huo, zaidi ya shilingi trilioni moja zitatumika na kunufaisha zaidi ya wanafunzi milioni 6.5 hadi utakapokoma mwaka 2025.”

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Serikali inatarajia kwamba programu ya iMBEJU itazalisha teknolojia mahsusi kwa ajili ya Watanzania.

“Wabunifu wa Kitanzania ndiyo wenye nafasi kubwa ya kuja na teknolojia zitakazotufaa Watanzania. Hii ni fursa kwetu kama tutatumia changamoto zetu kama chachu ya bunifu zetu kwa ajili yetu na tena tutaweza kuongeza soko kwa kupeleka bunifu kwa wale tunaoshindana nao,” alisema.

Akitoa salamu zake kwa washiriki, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dkt. Khalid Salum Mohamed alisema SMZ inashirikiana na Tanzania bara na sekta binafsi kukabiliana na changamoto za mawasiliano.

“Kupitia Serikali ya Muungano, TCRA, kampuni ya Tigo-Zantel na UCSAF tumefanikiwa kuweka minara 45 katika visiwa vya unguja na Pemba na hasa vijijini ambako kulikuwa na changamoto ya mawasiliano. Ujenzi uliofanyika ndani ya miezi mitatu na pia tunajenga vituo vya TEHAMA kwenye wilaya zetu zote 11. Kila wilaya inakuwa na kituo kimoja.”

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema katika programu ya iMBEJU watakuwa pia wakitoa mafunzo ya usimamizi wa biashara, matumizi ya mifumo ya TEHAMA, elimu ya fedha na masoko, na usaidizi wa kuboresha bidhaa na mawazo bunifu ambapo kwa kuanzia wametenga sh. bilioni tano.

“Vijana wanatakiwa kuwa na nidhamu ya fedha. Kupitia programu ya Imbeju, vijana watakuwa na nidhamu ya maisha, nidhamu ya fedha na nidhamu ya kibiashara.”

Kuhusu uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali, Nsekela alisema benki hiyo itakuwa ikifanya kazi na taasisi na mashirika yanayofanya uwezeshaji kwa wanawake. Uwezeshaji utafanyika kwa vikundi na wajasiriamali mmoja mmoja.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma