skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika inaadhimisha miaka 30 tangu kuasisiwa huku kukiwa na changamoto nyingi ikiwemo mbinyo wa kisheria dhidi ya uhuru wa kujieleza na hali duni kwa waandishi wa habari

Azimio la Windhoek la mwaka 1991 na baadaye kuanzishwa kwa Taasisi kwa MISA ndio ulioanzisha safari ya kudai uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza kama msingi sahihi wa ukuaji wa demokrasia baada ya nchi nyingi za bara la Afrika kupata uhuru

Akihutubia katika kongamano linalowaleta pamoja wadau pamoja na serikali, mwenyekiti wa MISA Tanzania Salome Kitomali amebainisha kuwa pamoja na mageuzi mbalimbali, tasnia ya habari inakabiriwa na hali ngumu kutokana na sheria zisizo rafiki ikiwemo hali ngumu ya maisha kwa waandish wa habari ambapo wengi waoo hawalipwi mishahara na stahiki nyingine za kiutumishi ikiwemo bima ya afya na kutokuwa na akiba mfuko wa jamii kunakosababishwa na waajiri kutowalipia watumishi wao katika vyombo vya habari.

Salome Kitomali Mwenyekiti wa MISA Tanzania akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya kuasisiwa kwa taasisi hiyo

Ombwe kubwa ambalo linalalamikiwa ni serikali kuchelewa kufanyia kazi maoni ya wadau hasa kuhusu kurekebisha sheria kandamizi sinazozorotesha uhuru wa habari nchini, hoja kuu ni je kwanini kumekuwepo na ugumu huo?

Edwin Soko ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya pamoja ya haki ya kupata habari maarufu CORI anabainisha kuwa changamoto kubwa ni namna taasisi zilivyokuwa zinashirikiana katika kudai haki hiyo, namna ya kuifikia serikali, pamoja na serikali yenyewe inavyoyapokea maoni ya wanahabari kuhusu mabadiliko yanayoombwa.

“Kuna namna sisi wenyewe hatujafanya vizuri katika kushirikiana kudai haki na uhuru wa habari, kuna kutoaminiana miongoni mwetu na pia serikali nayo haituoni kama wadau mhimu katika mchakato wa maendeleo ndiyo maana sheria ngumuu na mbaya zinatungwa bila kuangalia athari kwa upande wa pili na kwa jamii pia”. Anasisitiza Edwin Soko

Maadili ni moja ya maeneo yanayotajwa kuichochea serikali kutunga sheria kali dhidi ya vyombo vya habari, waasisi wa MISA Tanzania wanabainisha kuwa ipo kazi ya kuwaelimisha wanahabari kujitambua ili kuepuka makosa ambaayo yanaweza kupelekea vyombo kuingia matatani

kama maadili hayazingatiwi lazima serikali iingilie kati, haiwezi kuacha tu mambo yaende hovyo na inalazimika kuingilia ili jamii inufaike na huduma za habari” alisisitiza Rose Haji Mwalimu mwanamke wa kwanza kuwa mkurugenzi wa MISA Tanzania

Hata hivyo serikali ya Tanzania imetaja kuwa na nia thabidi ya kuboresha mazingira ya kazi za vyombo vya Habari na kwamba sheria zinazolalamikiwa iko tayri kuzirekebisha

Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ameweka bayana kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaonesha dhamira thabiti ya kuweka mazingira rafiki kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru

Moja ya alama ya dhamira ya serikali ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya kupitia changamoto cha vyombo vya habari iliyoundwa na Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari Moses Nnauye ambayo itachambua kwa kina na kutoa mapendekezo ambayo yatatumika kuipa fursa serikali na wadau wa habari kuimarisha utendaji wa vyombo vya habari.

Imebainika kuwa wiki hiii kamati ya Bunge ya katiba na sheria itakutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya kupokea maoni kuhusu marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo ya huduma za Habari.

Bi. Elizabeth Riziki mkurugenzi wa MISA Tanzania akizungumza na wadau wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya MISA

Uongozi wa MISA Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine ndani na nje ya nchi ikiwemo ofisi za MISA kanda wameelezea kuwepo kwa mikakati mbalimbali ya kuimarisha taasisi ili kuhakikisha jamii ya wanahabari na vyombo vya habari vinafanya kazi zake kwa uhuru na weledi

Mkurugenzi wa MISA Tanzania Bi. Elizabeth Riziki ameweka bayana kuwa Bodi ya MISA kwa kushirikiana na sekretariat inaendelea kuweka mipango imara ya maendeleo ya kitaasisi, na kuongeza wigo wa kufanya kazi na wadau wengine wakiwemo INTERNEWS, UNESCO, IMS, FNF, SDC, na FREEDOM HOUSE.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma