skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mussa Mkilanya

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema katika mkoa wake jambo kubwa linalomnyma usingizi ni mauaji yanayotokana na migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Kunenge ameyasema hayo katika kikao maalum cha mpango kazi cha kutafuta ufumbuzi wa namna ya kumaliza migogoro hiyo ili kukomesha ifo vinavyotokana na mapigano ya wakulima na wafugaji.

Amesema Mkoa wa Pwani umedhamiria kumaliza tatizo la Migogoro baina ya Wakulima na Wafugaji, tatizo ambalo limedumu kwa muda mrefu katika mkoa huo, kutokana na kuwepo kwa makundi makubwa ya mifugo yanayotokana na watu kuvamia maeneo kutoka katika mikoa mingine kwa ajili ya malisho.

Kunenge, amesema Mkoa huo umepata changamoto za vifo vya mara kwa mara, watu kupata ulemavu na kuzorota kwa shughuli mbalimbali za maendeleo hali inayosababishwa na changamoto hiyo.

Aidha Kunenge amesema, amebaini kuwa wapo baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanachochea migogoro hiyo kwasababu wanamaslahi yao.

Hata hivyo ameonya watu ambao wanatumiwa kama vivuli na viongozi wanaomiliki idadi kubwa ya mifugo, kutotenda makosa ya kulishia mifugo katika mashamba ya watu wakitarajia kupata msaada kutoka kwa wamiliki wao.

Amesema watu wengi wamefariki na wengine kupata ulemavu wa kudumu kutokana na kutoipatia ufumbuzi migogoro hiyo, huku akiahidi kuwa uongozi wa Mkoa wa Pwani uliyopo sasa hautafumbia macho wala kumuogopa mtu yeyote.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bi. Zainab Abdallah amesema kutokana na kukithiri kwa migogoro hiyo, wamekuwa wakikosa muda wa kushughulikia maswala mengine ya kimaendeleo kutokana na kutumia muda mwingi katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo.

DC Zainab, amezitupia lawama baadhi ya taasisi za serikali, zikiwemo mahakama, Ofisi za Takukuru kwa kutoshughulikia taarifa za kihalifu wanazozipata kwa wakati.

Amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha hofu kubwa kwa wakulima ambao wengi ni watu wakipato cha chini tofauti na ilivyo kwa wafugaji.

Hata hivyo Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema, sasa umefikia wakati kila kiongozi wa Serikali asimamie sharia za nchi, kwani kufanya hiyo kutasaidia hata watu wanaohamia katika eneo fulani kutambuliwa kirahisi pamoja na idadi ya kifugo waliyonayo.

Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza idadi ya wafugaji  wanaovamia maeneo katika Mkoa wa Pwani na kupunguza migogoro inayotokana na wakulima na wafugaji.

Hata hiyo George Kifuko ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya chama cha wafugaji anayeshughulikia migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa Aridhi na malisho Tanzania na Sefu Ally Njela, mkulima kutoka kijiji cha Jaribu Mpakani Kata ya Mjawa Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani, wamesema kuwa hata wao hawapendi kuona vifo vinavyotokana na migogoro baina ya wakulima na wafugaji, hivyo wapo tayari kuiunga mkono Serikali endapo inadhamira ya dhati katika kukomesha migogoro hiyo.

Sikiliza ripoti kuhusu habari hii, usikie maagizo na nasaha za viongozi wa mkoa wa Pwani. Bonyza pichani hapo chini.

Taarifa kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji kutoka Pwani- ni funzo kwa mkoa wa Kigoma

Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa maeneo ambayo hivi karibuni yamepokea wakulima na wafugaji wenye maelfu ya mifugo kutoka mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Tabora na tayari kumeibuka migogoro baina yaoo na wenyeji jambo linalohitaji ufumbuzi wa mapema ili kuepusha maafa kama yanayoripotiwa katika Mikoa ya Pwani na Morogoro.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma