skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Sungura Jeremiah

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu ajira, vijana na wenye ulemavu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la kasulu mjini mhe. Prof Joyce Ndalichako amefanya mkutano na wakazi wa Mji wa Kasulu Kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020.

Katika mkutano huo wa hadhara ambao uliudhuriwa na viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mji, wakuu wa idara mbalimbali, mashirika yasio ya kiserikali, vyombo vya habari, Mbunge alitaja miradi ya kimkakati ambayo imetekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu alipochaguliwa.

Profesa Ndalichako ameeleza kwa kina namna alivyoboresha sekta ya Afya wilayani kwa kujenga vituo vipya vya afya viwili katika kata ya Nyansha na Heru juu, Zahanati mpya sita katika mitaa ya Kumnyika, Nyansha, Msambara, Kabanga na Ruhita

Amebainisha kuwa katika afua ya Afya, serikali imewezesha ujenzi wa nyumba za waganga na wauguzi ili kuwezesha upatikanaji huduma za afya kwa wanachi wakati wote.

Aidha Profesa Ndalichako ameweka bayana kuwa kupitia katika mpango maalumu wa maboresho ya huduma za afya na rufaa ya wagonjwa, Kasulu umejengewa jingo maalumu la wagonjwa mahututi lenye vifaa vitakavyotoa huduma za kibingwa na hivyo kuwapunguzia wananchi usumbufu wa rufaa Kwenda hospitali ya Mkoa wa Kigoma (maweni) na Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza

Pia, ameeleza jitihada kubwa azilizofanywa kuboresha sekta ya elimu wilayani ikiwa ni Pamoja na ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (VETA) Nyumbigwa na chuo cha Watoto wenye ulemavu ambacho pia kimejengwa katika Mtaa wa Nyumbigwa mjini Kasulu.

“Jitihada kubwa imefanyika katika kuendeleza na kuboresha sekta ya elimu katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni Pamoja na ujenzi wa shule moja ya elimu ya juu (A-LEVEL), Ujenzi na ukarabati wa shule za msingi na sekondari, kuongezwa na kutengenezwa kwa madawati zaidi ya 1000 ambayo sehemu kubwa yameshasambazwa katika shule kadhaa na mengine yatagawiwa kwa shule zenye uhitaji mkubwa hivi karibuni”

Mbunge huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa wa uchapa kazi na ufuatiliaji wa  shughuli za maendeleo nchini, amewaahidi na kuwataka wakazi wa Kasulu kuendelea kuwa na imani na serikali yao chini ya mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa barabara na reli ya kiwango cha kati (standard Gauge) inayojengwa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Tabora hadi Kigoma.

“Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi sana, na hapa nitoe siri kwenu wananchi wa jimbo langu, katika mpango wa reli ya kisasa kutoka Uvinza Kwenda Burundi, kitajengwa kituo cha abiria katika eneo la Kata ya Nyasha, na kitakuwa kituo kikubwa na cha kisasa, nani kama mama Samia?” alisisitiza Prof. Ndalichako katika hotuba yake

Profesa Ndalichako (Mbunge) akisalimiana na mmoja wa wananchi wa Kasulu Mjini ambaye aliwasilisha hoja na malalamiko yake kwa Mbunge kuhusu masuala mbalimbali ya huduma za jamii ambayo yana changamoto. Aidi ya watu 30 walipata fursa ya kutoa maoni, kuuliza maswali na kupata majibu

Akikiri mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika sekta ya umeme mhe. Mbunge amewataka wanachi kuendelea kuwa wavumilivu kwani serikali ya awamu ya sita inatambua uwepo wa miundombinu mibovu ya umeme nchini, na kwamba tayari mkoa wa Kigoma umeunganishwa na gridi ya Taifa kutokea Nyakanazi hadi Buhigwe na ujenzi wa miundombinu ya uhakika unaendelea ili kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara

Wananchi kwa upande wao wameonyesha kuvutiwa sana na kile ambacho mbunge wao amekuwa akikifanya katika kuhakisha wanapata na kutimiziwa haja zao kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.

Aidha wenyeji hao walitoa malalamiko yao na kero zao hasa suala ya Urasimishaji Ardhi ambao serikali imekuwa ikifanya bila jamii kuwa na elimu juu ya suala hilo

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kasulu alitoa wito kwa wananchi wenye kero na hoja mbalimbali kufika ofisini kwake wakiwa na vielelezo ili halmashauri izifanyie kazi na kutatua kero zao badala ya kusubiri mikutano ya mbunge.

Sambamba na majibu kwa kero za wananchi, Prof ndalichako ametoa wito kwa watumishi wa umma kutambua kuwa wao ni watumishi wa wananchi na kila mwajiriwa wa serikali anatakiwa kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa kuzingatia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya nane na miongozo mingine ya kiutumishi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma