skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Philp Mpango amewaagiza wakimbiza Mwenge kitaifa kutozindua au kuweka mawe ya msingi pamoja na kufungua miradi ambayo itabainika kutolingana na thamani ya pesa zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wake.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizindua mbio za mwenge wa uhuru kitaifa zilizofanyika mjini Njombe mapema leo akisisitiza kuwa serikali inatoa pesa ili miradi inayotekelezwa ilingane thamani na pesa hizo ambazo ni kwa ajilii ya maendeleo ya wananchi

“Nawaagiza wakimbiza Mwenge, msiende kuweka mawe ya msingi, au kuzindua au kufungua mradi wowote mtakaokuta una mapungufu ya aina yoyote, jiridhisheni kwanza na kama mtabaini kuwepo kwa dosari yoyote toeni taarifa kwa vyombo vinavyohusika ili hatua mbalimbali zichukuliwe haraka dhidi ya wahusika” amesisitiza Dr. Mpango Makamu wa Rais

Akitoa ufafanuzi kuhusu ujumbe wa mbio za mwenge, Mheshimiwa Mpango amesisitiza kuwa mwaka huu ni mwaka ambao Tanzania itafanya sensa ya watu na makazi, hivyo kila mwananchi ajitokeza kuhesabiwa ili serikali ifahamu idadi ya watu wake, shughuli zao na makazi yao kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya taifa.

Kuhusu Ukimwi, Dr. Mpango ametoa wito kwa jamii kutojisahau wakaidhani UKIMWI haupo badala yake waendelee kuchukua tahadhali, huku akiutaja mkoa wa njombe kuwa ndio wenye kiwango cha juu cha maambukizi ukifuatiwa na mkoa wa Iringa na Mbeya kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2021

“Endeleeni kudhukua tahadhari, ukimwi bado upo, sisi kwa upande wetu serikali tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti maambukizi, hivyo ni jukumu la kila mtanzania kuwa makini” Alisisitiza Dr. Mpango

Kuhusu masuala ya lishe, Dr. Mpango amebainisha kuwa licha ya mikoa ya nyanda za juu kusini na magharibi kuwa katika kundi la mikoa inayozalisha chakula kwa wingi, bado kuna tatizo kubwa la udumavu kwa watoto unaotokana na lishe duni.

ameitaja mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa Katavii na Kigoma kuwa na kiwango cha juu cha udumavu jambo linaloshangaza taifa na kwamba inatokana na ulaji usiozingatia kanuni za afya na lishe.

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu Prof. Ndalichako amebainisha kuwa wizara yake imeandaa vijana wakimbiza mwenge wenye sifa thabiti ambao watakidhi malengo ya mbio za mwenge mwaka 2022.

Profesa Ndalichako amemhakikishia Mhe. Makamu wa Rais kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya habari, vijana utamaduni na Michezo Zanzibar watahakikisha kwamba shughuli zote zilizopangwa kwa ajili ya mbio za mwenge zinaenda kama zilivyopangwa, ikiwemo kuhakikisha mwenge unakuwa ni chachu ya mageuziz ya kijamii na kufanikisha dira ya Sensa ya watu na makazi.

“Mheshimiwa makamu wa Rais,mbio za mwenge wa uhuru ziliasisiwa na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere baada ya Tanganyika kupata Uhuru kutoka kwa ukoloni wa Uingereza tarehe 9 Disemba mwaka 1961, na tangu zilipoasisiwa, mbio za mwenge zimeendelea kudumisha uhuru wetu, amani, mshikamano, uzalendo na ni kichocheo cha maendeleo kwa wananchi” Amesisitiza profesa Ndalichako.

Amesisitiza kuwa, kupitia mbio za mwenge wananchi wamekuwa wakihamasishwa kuhusu mambo ya kitaifa, kubuni na kuendeleza miradi ya maendeleo na mwenge umekuwa ni kichocheo kwao.

Profesa Ndalichako amebainisha kuwa kutokana na ujumbe wa mbio za mwenge msukumo mahususi umekuwa ukitolewa katika masuala maalumu, na kwamba ujumbe wa mio za mwenge wa Uhuru mwaka huu unajikita katika kuhakikisha jamii inajikinga na malaria, kupinga na kuzuia matumizi zya madawa ya kulevya, Lishe, Usawa wa kijinisa, na mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi

Mbio za mwenge wa Uhuru zitahitimishwa mkoani Kagera Oktoba 14 mwaka huu baada ya kukimbizwa katika mikoa 31 na halmashauri 195.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2022 ni ndugu Sahili Nyanzabara Gararuma kutoka mkoani Njombe

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma