Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kama ifuatavyo:…
Na Anita Balingilaki, Bariadi
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga amepiga marufuku kwa watumishi wa serikali na viongozi wa kuchaguliwa wilayani hapo kuomba na kupewa zabuni (tender) au kusambazaji vifaa vya ujenzi kwenye miradi ya serikali.
Amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya afya inayotekelezwa kwenye halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu ambapo ameongeza kuwa hata kanuni ya maadili hairuhusu.
Simalenga amesema hali hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha miradi kusuasua huku mingine ikijengwa chini ya kiwango kwani ni ngumu msambazaji au mshika zabuni (tender) kujikagua
” Ni marufuku kwa kiongozi yeyote wilayani hapa awe ni wa kuchaguliwa au ni mwajiriwa kuchukua tender ya kusupply chochote kwenye ujenzi wa majengo ya serikali yaani hapo tunaanza na mwenyekiti wa kitongoji,mwenyekiti wa kijiji,mtendaji wa kijiji/ kata, diwani kwenda mpaka ngazi ya halmashauri yenyewe sitaki kusikia mtu amechukua tender yakusupply au kujenga chochote kwenye mradi wa serikali”Simalenga.
Katika hatua nyingine Simalenga akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo matatu ya hospitali ya halmashauri ya mji wa Bariadi amewataka kuhakikisha yanakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji ujenzi wa majengo hayo mganga mfawidhi hospitali ya halmashauri hiyo Dkt Rose Mushi amesema kiasi cha shilingi milioni 900,000,000 zilipokelewa Septemba 19,2022 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi huo.
Majengo hayo ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje ( OPD), jengo la upasuaji na jengo la maabara ambapo ujenzi ulianza Oktoba 28,2023 na mradi huo utachukua muda wa miezi sita, mbali na ukamilishaji fedha hizo zinatumika kukarabati wodi no 1,2,3B na 4 hospitalini hapo.

Kuhusu utekelezaji wa mradi huo Dkt Mushi amesema utakuwa wa awamu mbili,awamu ya kwanza ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) maabara na jengo la upasuaji huku awamu ya pili ikihusisha ukarabati wa wodi no 1, 2, 3B na 4 kulingana na kiasi cha fedha kitakachosalia baada ya kukamilisha ujenzi wa majengo matatu.
Amesema majengo ya maabara na upasuaji yapo katika hatua za ukamilishaji huku jengo la wagonjwa wa nje (OPD) likiwa katika hatua ya upauwaji.
” Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) limefikia asilimia 70, maabara asilimia 80 na jengo la upasuaji asilimia 85″amesema Dkt Mushi.
Kuhusu mchanganuo wa fedha Dkt Mushi amesema kiasi cha shilingi milioni 703,616,450 kimeshatumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi, kiasi kilichobaki ni shilingi milioni 196,383,550 kati ya shilingi milioni 900,000,000 zilizopokelewa.