skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya nchini wasimamie ajenda za kitaifa ikiwemo ya mapambano dhidi ya rushwa ili kuleta maendeleo chanya kwa wananchi katika maeneo wanayoongoza.

Amewataka pia washirikiane na wadau kutatua changamoto za upatikanaji wa ajira, kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kusimamia uoto wa asili na kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji sambamba na usimamizi wa miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato ya Serikali na utatuzi wa kero za wananchi.

Ametoa wito huo leo jana wakati akifunga Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya 138 yaliyofanyika kwenye ukumbi wa St. Gasper, jijini Dodoma ambao ni mpango wa serikali kuhakikisha watendaji na wasimamizi wa shughuli za serikali wanazingatia maadili na uwajibikaji.

Waziri mkuu Kassim Majaliwa akuwahutubia wakuu wa wilaya nchini wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan

Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wakuu hao wa wilaya kukabiliana na tatizo la rushwa, kwa kukemea na kufuatilia mianya ya rushwa ili izibwe na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila kulazimishwa kutoa rushwa.

Akiwakumbusha wajibu wao, Waziri Mkuu amewataka wakuu hao wa wilaya wafuate maagizo na maelekezo ya mamlaka iliyowateua na akawataka watambue kuwa wao ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais kwenye maeneo yao.

Aina ya utumishi huu wa uteuzi ni tofauti na ule wa mchakato wa usaili, kwa hiyo mnapaswa kutambua mwenye mamlaka anataka nini, mnapaswa kuenenda na maono yake, matakwa yake na maelekezo yake, Ili mradi umeteuliwa na umeapa, wewe ni kiongozi wa Serikali wa eneo ulilopewa na ni msimamizi wa shughuli zote za Serikali na hata za sekta binafsi. Kwa hiyo unalo jukumu la kufuatilia na kujiridhisha je, yanayofanywa na sekta binafsi yanalenga kuleta maendeleo?” amesisitiza.

Akielezea umuhimu wa majukumu yao, Waziri Mkuu amesema: “Tunapozungumzia maendeleo ya nchi, hatuwezi kuyafikia bila uwepo wenu kwa sababu ninyi ndiyo wenye watu. Kuna wilaya ina Halmshauri moja nyingine mbili au tatu. Ni lazima ufuatilie yanayoendelea katika wilaya yako na matarajio ya Mheshimiwa Rais ni kuona kuwa mtawahudumia wananchi, mtawatumikia na kusikiliza kero zao.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakuu hao wa wilaya, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Angellah Kairuki alisema mafunzo hayo ya siku sita yaliyoanza Machi 13, mwaka huu yalihusisha washiriki 139 ambapo kati yao 37 ni wapya na wengine 102 ni wale wanaoendelea na nyadhifa zao.

Hayo ni mafunzo ya pili kwa viongozi wa kuteuliwa na Rais, baada ya kumalizikwa kwa mafunzo ya Mawaziri, manaibu wao, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara zote yaliyofanyika mjini Arusha mwezi huu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma