skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Kifo cha mama mzazi wa Mbunge wa jimbo la Kasulu mjini na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, ajira na wenye ulemavu Profesa Joyce Ndalichako kimeibua mengi yaliyokuwa nyuma ya pazia la maisha yake na kuacha gumzo kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma.

Hayo yamebainishwa leo nyumbani kwa marehemu eneoo la Nazareth mjini Kigoma na paroko wa kanisa kuu Katoliki Jimbo la Kigoma, Padre Kastus Rwegoshora wakati wa mahubiri ya ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Mary Ivo Ndalichako aliyefariki dunia jumamosi May 21 jijini Dar salaam

Padre Kastus Rwegoshora (mwenye Biblia) akiongoza sala ya kumuombea Marehemu Mary Ivo Ndalichako, wa kwanza kushoto ni Padre Venance Ndalichako mtoto wa Marehemu pamoja na ndugu zake

Padre Rwegoshora amebainisha kuwa, ni nadra kukuta mtu akiwa na chumba maalumu cha sala nyumbani kwake kama alivyofanya mama Mary Ndalichako ambaye alitenga moja ya vyumba vya nyumba yake kuwa kanisa dogo ambapo alisali kila siku pamoja na kuhudhuria misa za asubuhi katika kanisa la Katubuka mjini Kigoma.

Marehemu Mary Ivo Ndalichako

Huyu mama ametuachia funzo kubwa, alimpa Mungu nafasi kubwa katika maisha yake, na ametuachia zawadi kubwa ya mtoto ambaye ni Padre pamoja na mwingine ambaye ni Waziri, hakika ametimiza wajibu wake vizuri, amewaonesha njia watoto wake kwa malezi mema na sasa anatangulia kwenda kuwaandalia makao na atawapokea huko” Alisisitiza Padre Rwegoshora.

Padre Rwegoshora amebainisha kuwa binadamu wengi tunajiwekea hazina na fursa nyingi za duniani na hatumkumbuki Mungu, wengi huandaa vyumba vya TV, vyumba vya magazeti nk na hatuweki maeneo maalumu ya ibada ndani ya nyumba zetu.

Familia ya Marehemu mary wakiongozwa na Profesa Joyce Ndalichako na Padre Evance Ndalichako wakiuaga mwili wa mama yaoo katika chumba ambacho alikitumia kwa ajili ya Ibada wakati wa uhai wake

Akisoma taarifa fupi ya Marehemu Mary Ivo,, Mtoto wake ambaye ni Padre Venance Ndalichako amebainisha kuwa licha ya mama yao kuwa mzazi, mlezi na mwalimu kitaaluma, aliwalea watoto wake katika maadili na alikuwa sii mwalimu wa shuleni tu bali hata katika familia yake.

Mary Ivo Ndalichako alifanikiwa kupata watoto 10 watano (5) wa kiume na watano wa kike na ameacha hai watoto wanane kati yao na wajukuu na vitukuu.

Kwa upande wake Profesa Joyce Ndalichako katika hatua za awali, amewashukuru watu mbalimbali waliojitokeza katika kiwanja cha ndege Kigoma, kushiriki ibada nyumbani kwa Marehemu na kumsindikiza hadi kasulu ambapo atapumzika katika makazi yake ya milele

Ndugu, Jamaa na marafiki wakiongozwa na Profesa Ndalichako na Askofu msaafu wa kanisa la Anglikana Sadock Makaya wakiaga Mwili wa mpendwa waoo Nyumbani Nazareth Kigoma.

Mazishi wa marehemu Mary Ivo Ndalichako yatafanyika kesho May 25 katika makaburi ya Mtakatifu Fransis Exavery Kasulu baada ya kuwasili kutoka Dar es Salaam kupitia Kigoma ambako aliagwa nyumbani kwake Nazareth parokia ya Katubuka.

Kabla ya mazishi itafanyika ibada ya kumuaga marehemu katika Kanisa katoliki kigango cha Mtakatifu Paul Mwilamvya parokia ya Kasulu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma