skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

Shule ya Msingi Mwanga yenye takribani wanafunzi 2000 iliyopo manispaa ya Kigoma Ujiji inakabiliwa na uhaba wa madawati pamoja na uhaba wa walimu unaoendana na uwiano wa wanafunzi waliopo.

Akizungumza Robert Lubungila mwalimu mkuu wa shule ya Mwanga  amesema shule hiyo ina upungufu wa madawati 600 hali inayolazimu idadi kubwa ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini.

Vilevile mkuu wa shule hiyo amesema kuna upungufu wa walimu 10 wanaihitajika ili kukidhi haja ya kila mwalimu kufundisha wanafunzi angalau 60-70 jambo ambalo bado lina kinzana na sera ya elimu ya mwaka  2014 inayoelekeza mwalimu mmoja  kufundisha wanafunzi 45.

“Shule yangu ina walimu 26, ili angalau mwalimu mmoja aweze kufundisha wanafunzi 60 au 70 inatakiwa nipate ongezeko la walimu 10 kutoka idadi iliyopo ili waweze kumudu ufundishaji bora” Amesema Lubungila.

Hali halisi inatakiwa kuwa na uwiano wa dawati moja kwa wanafunzi watatu hadi wanne kwa nchi nzima jambo ambalo ni tofauti kwa shule ya msingi Mwanga ambapo kwenye dawati moja wanakaa mpaka wanafunzi saba

Sarah Munsari mwanafunzi wa darasa la saba wa shule hiyo amesema wanapata changamoto kwenye kuandika vizuri na kusikiliza kwa makini kile wanachofundishwa kwasababu wanakuwa wamebanana wakati wa ufundishwaji.

Wanafunzi wakiwa wameketi chini darasani kutokana na uhaba wa madawati mkoani Kigoma

Naye Elia Fred mwanafunzi wa darada la tano amesema kuwa wengi wa watoto wanaokaa chini hasa wa kuanzia darasa la tatu hadi chekechea wanakuwa si nadhifu kwasababu ya nguo zao kuwa chafu kila siku huku baadhi ya wazazi wakishindwa kufua kutokana na haba wa sabauni

Akiongea kwa niaba ya wazazi Dorothea Kapaya ameiomba serikali pamoja na taasisi zinazosimamia sera za elimu bora kuhakikisha wanatafuta mbinu za kupata madawati pamoja na miundombinu mingine kama ya vyoo na nyumba za walimu ili wanafunzi waweze kufaulu zaidi katika masomo yao.

Akizungumia changamoto hizo Richard Mtauka afisa elimu msingi manispaa ya Kigoma Ujijji amesema serikali ipo inajenga vyumba vya madarasa 53 kupitia mradi wa Boost wenye gharama za shilingi bilioni 1.2 ili kuhakikisha wanafunzi wanaoandikishwa wanapata maeneo ya kukaa

Amesema mradi wa “BOOST” utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa miundombinu ya madarasa na madawati kwa asilimia 51 unaozikabili shule za msingi za manispaa hiyo.

“Licha ya changamoto zilizopo uandikishaji wa watoto kwa madara ya awali na msingi umefikia zaidi ya asilimia 95 na kwa matokea ya darasa la saba kwa mwaka 2022 ufaulu ulikuwa asilimia 86.4 ambacho ni kiwango cha alama za juu” Amesema Mtauka

Kwa mujibu wa afisa elimu huyo manispaa ya Kigoma Ujiji  ina upungufu wa walimu 428 katika shule 54 zilizopo.

Ushirikiano wa pamoja baina ya wadau wa maendeleo, serikali na wananchi unahitajika ili kutatua changamoto ya upungufu wa madawati, uhaba wa walimu, nyumba za walimu na ongezeko la watoto wanaojiunga darasa la kwanza na kitado cha kwanza kila mwaka.

Wito unatolewa kwa maafisa vifaa na takwimu kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha takwimu sahihi zinakuwepo ili kuongoza jami katika kupanga mahitaji ya elimu kila mwaka.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma