skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki,Simiyu

Katika kuhakikisha jamii inafikiwa kwa ukaribu na kupata huduma za afya za kibingwa zaidi ya madaktari bingwa 24 wanatarajiwa  kupiga kambi mkoani Simiyu.

Hayo yamesemwa na mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu Dkt Athanas Ngambakubi wakati akiongea na waandishi wa habari akiwa hospitalini hapo.

Dkt Ngambakubi amesema kambi ya madaktari hao inaitwa  mama Samia Suluhu Hassan na  itahusisha madaktari bingwa kutoka kanda ya ziwa na itafanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu kuanzia June12 hadi June 16, mwaka huu.

Amesema madaktari bingwa hao ni kutoka fani mbalimbali wakiwemo wa magonjwa ya watoto, wanawake, kinywa,pua,masikio,mifupa,afya ya akili na upasuaji kwa ujumla.

Madaktari hao wanatoka hospitali ya rufaa ya kanda ya Bugando,hospitali ya mkoa wa Mwanza Seketure,hospitali ya mkoa wa Mara,hospitali ya mkoa ya Shinyanga,hospitali ya mkoa wa Geita,hospitali ya mkoa wa Kagera na watashirikiana na madaktari bingwa waliopo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu.

Aidha amesema wagonjwa wote watakaofika hospitalini hapo watahudumiwa ikiwa ni sambamba na kupunguzwa kwa gharama zikiwemo za kumuona Daktari.

Nao baadhi ya wananchi hususan kutoka wilaya ya Bariadi wamepongeza kusogezewa huduma za kibingwa karibu na maeneo yao ambapo wamesema kuwa itakuwa msaada mkubwa wa kupunguza gharama za matibabu na usafiri na itachochea idadi kubwa kufika kupata huduma za kiafya.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma