Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kama ifuatavyo:…
Na. Anitha balingilaki, Simiyu
Jumla ya shilingi bilioni 14.9 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi 24 ya maji mkoani Simiyu na kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji wa maji mkoani hapo kutoka asilimia 70.50 hadi kufikia asilimia 73.10 ifikapo disemba 2023.
Hayo yamesemwa na meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA) mkoa wa Simiyu mhandisi Mariam Majala wakati akitoa taarifa ya
huduma ya maji mkoani hapo katika hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya ujenzi
wa skimu za maji kwa mwaka 2022/23 iliyofanyika wilayani Bariadi.
“RUWASA mkoa wa Simiyu katika kipindi cha mwaka 2022/2023 uliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 14.9 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji ya bomba 15, Bariadi 10, Busega 1,Itilima 1, Maswa 2 na Meatu 1…mkoa unatarajia kuchimba virefu visima 28..Bariadi 10, Itilima 4, Maswa 10 na Meatu 4 ikiwa ni vyanzo vya maji kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi…kukarabati na kununua pump za mkono 240” amesema mhandisi Majala na kuongeza kuwa:

” Kati ya miradi ya maji 24 inayotarajiwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/23, miradi 8 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 4.09 taratibu za manunuzi zimekamilika na ipo tayari imesainiwa kwaajili ya utekelezaji…miradi mingine 16 itasainiwa baada ya taratibu za manunuzi kukamilika” ameongeza mhandisi Majala .
Awali mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed akatoa rai kwa wakandarasi wote ambao wamesaini mikataba wakatekeleze kwa wakati na sio kusumbua serikali kuwafatilia na chama kuwakagua mara kwa mara huku mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda akaagiza miradi hiyo isimamiwe
kikamilifu na ikamilike kwa wakati kwa kuzingatia ubora ili idumu kwaajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
” RUWASA endeleeni kusimamia miradi hii na iwe katika hali ya viwango vya juu sana, na kwa uhakika hamuwezi kutuangusha… fedha ni nyingi, mmeona kwa miaka miwili mheshimiwa Rais ametuletea zaidi ya shilingi bilioni 35 katika miradi ya maji, kwahiyo tunataka hii miradi ikawe chachu ya kupunguza adha katika wilaya zetu na katika vijiji vyetu, na hiyo miradi idumu miaka 100 baadaye ili mwisho wa siku fedha za serikali zionekane thamani halisi.” amesema Dkt. Nawanda na kuongeza kuwa:
“Ndani ya mkoa wa Simiyu miongoni mwa miradi inayofanya vizuri ni miradi ya RUWASA kwa hiyo najua hata hii itafanyika vizuri”ameongeza Dkt Nawanda.
Regina Masatu ni mwenyekiti wa wakandarasi mkoa wa Simiyu kwa niaba ya wenzake ameahidi kuwa watatekeleza miradi hiyo kwa wakati.
“Sisi kama wakandarasi na wasambazaji tunapenda kutoa shukrani kwanza kwa kutuamini na leo mbele yenu tunakiri kwamba hii kazi mliyotupatia tunakiri pia kwa wale walengwa huu mradi unaenda kuwafikia tutafanya kazi kwa bidii lakini pia tutafanya kwa weledi na tunaahidi kwamba tutamaliza kwa wakati.” amesema Masatu.