skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Simiyu

Mkoa wa Simiyu umepania kuhakikisha kiwango cha wagonjwa wanaoambukizwa kifua kikuu kinashuka na kuwezesha wagonjwa kupata matibabu ya uhakika kama sehemu ya kutokomeza magonjwa ya kifua kikuu na ukoma katika mkoa huo wa kanda ya ziwa Victoria

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Simiyu Simiyu Bw. Emmanuel John wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari mkoani Simiyu juu ya namna bora ya kuripoti habari kuhusu ugonjwa huo kwa mkoa wa Simiyu.

Mratibu huyo ameweka bayana kuwa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu mkoani hapo kwa mwaka jana kulikuwa na wagonjwa 3600 ikilinganishwa na mwaka juzi ambapo walikuwepo wagonjwa 2700.

Bw. John amesema sababu za ongezeko hilo ni pamoja na shughuli mbalimbali ambazo zinafanywa na mkoa huo kama vile uibuaji wa wagonjwa kwa kutumia mobile van, matumizi ya x-ray machine ambayo inakuwa kwenye hilo gari hilo (mobile van) , wameboresha huduma kwa kuwafikia watu kwa urahisi hususan maeneo ya vijijini kwa kutumia hiyo maabara tembezi.

Mratibu huyo ametaja sababu zingine za ongezeko la wagonjwa wa kifua kikuu kuwa ni shughuli mbalimbali za kiuchumi hususan kambi za wavuvi wilayani Busega na uchimbaji mdogo wa madini kwenye maeneo mbalimbali mkoani hapo.

Mbali na kuwasogezea huduma karibu John amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wapate uelewa dhidi ya ugonjwa huo hatua itakayopelekea kufika kwenye vituo vya kutolea huduma kufanya uchunguzi na wakigundulika wana maambukizi waanze matibabu mapema ili kupunguza kuendelea kuambukizana kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwengine.

Kuhusu mkakati ambao mkoa unaona kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu ni kuwaibua watu ambao wanaishi na maambukizi ya kifua kikuu na kuwaweka kwenye matibabu na kuhakikisha wanazingatia miongozo ya Tiba.

Tanzania itaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya kifua kikuu kesho marchi 22 ambayo kitaifa yatafanyika mjini Bariadi mkoani Simiyu

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema ” kwa pamoja tunaweza kutokomeza kifua kikuu nchini Tanzania”

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma