skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane – Kigoma

Mshiriki wa mafunzo ya sensa inayotarajia kufanyika Agosti 23, 2022 Hadija Takato amewataka wananchi wa nchi jirani kutokuwa na hofu ya kuhesabiwa endapo watakutwa nchini usiku wa kuamkia siku hiyo.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma katika maadhimisho ya kuhitimisha mafunzo kwa wakufunzi wa sensa ngazi ya mkoa yaliyofanyika kwa muda wa majuma matatu na kuhitimishwa leo Julai 26, katika ukumbi mdogo wa shirika la hifadhi ya jamii (NSSF)

Amesema Kigoma imepakana na nchi ya Burundi na demokrasia ya Kongo hivyo ni rahisi kwa baadhi ya wananchi kutoka katika nchi hizo kuwemo nchini kwa malengo tofauti na kuwatoa hofu kwani watahesabiwa kulingana na kanuni na taratibu za nchi.

“Lipo gelesho maalumu kwa wananchi wa kigeni kuhesabiwa kama raia wa nchi husika,sensa haizuii kumuhesabu mtu ambaye ni mgeni, kiuhalisia wageni wanaweza kuogopa wakidhani wanataka kurudishwa kwao lakini nawatoa hofu kwakuwa hilo sio lengo la sensa” Amesema Takato

Kwa upande wa wananchi Jackson Kiza amesema yupo tayari kuhesabiwa ili kuirahisishia serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake na kusisitiza kuwa raia wa kigeni waliopo nchini kihalali watahesabiwa ila waliopo kinyume na taratibu ndio wanaoweza kujificha ili wasihesabiwe na hivyo serikali iangalie namna ya kuwapata.

Hata hivyo baadhi ya wanachi akiwemo Peri Simon mkazi wa manispaa ya Kigoma ujiji amekuwa na hofu baada ya kuambiwa kuna kutaja umri wakati wa kuhesabiwa na kuhoji kwanini wajulikane umri wao kwakuwa ni siri ya mtu na haina ulazima wowote

Akiwatoa hofu hiyo Thobias Yohana mkufunzi wa sensa aliyehitimu mafunzo yake, kutoka halmashauri ya wilaya ya Kasulu amesema kuwa lengo la kutambua umri ni pamoja na kupanga mahitaji kulingana na kundi rika fulani ikiwemo huduma za afya kwa wazee na elimu kwa watoto

Amesisitiza kuwa sensa itasadia serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

“Tunaendelea kutoa elimu katika mikutano na kwa mtu mmoja mmoja kuhesabiwa, hata kama ni wafanyakazi kutoka nchi jirani wanaofanya mashambani watahesabiwa lengo ni kupata takwimu sahihi za watu walioalala nchini usiku wa tarehe 22 Agosti kuamkia 23 Agosti, na wote watahesabiwa mara moja bila kujali umbali wa eneo husika”Amesema Yohana

Kwa upande wa wakufunzi wa mafunzo hayo Ibrahim Sogota amesema zaidi ya wanafunzi 300 waliohitimu kwa wastani wa asilimia 72 kwa nadharia na vitendo wanapaswa kwenda kuwafundisha makarani na wasimamizi ili wapate elimu kama yao kwani wao ndio mahususi katika kukusanya taarifa hizo muhimu.

“ Hili ni zoezi la kitaifa ambalo hufanyika mara moja baada ya miaka 10, linatumia pesa nyingi hivyo muwaelekeze makarani wakafanye zoezi hilo kikamilifu ili kuufanya mkoa wa Kigoma kuibuka kidedea” Amesema Sogota

Naye Mratibu wa sensa na makazi mkoa Kaheto Kahero amesema timu yake ipo mahiri na wamefuzu vizuri kutoa elimu ngazi ya tarafa na kata itakayoanza Julai 29, 2022 na kuwaomba makarani, wasimamizi na viongozi wa serikali kutoa ushirikiano ili kukamilisha suala hili kikamilifu

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma