skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

Wananchi wa kijiji cha Kagerankanda wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamelalamika kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi kutokana na kutokuwa na umeme wa uhakika na kuiomba serikali kuwaingiza kwenye umeme wa gridi ya Taifa.

Wametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya wabia wa maendeleo pamoja na wakala wa nishati vijijini REA yenye lengo la kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa nishati vijijini ambapo wananchi hao wamesema kampuni ya Engie Power Corner inayotoa huduma ya umeme wa sola kijijini hapo imeshindwa kutoa huduma ya umeme unaokidhi mahitaji yao na hivyo kuomba Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuingilia kati kwa kuwapatia umeme wa uhakika

Aston Albert mkazi wa kijiji hicho ambaye anafanya kazi ya kuchomelea amesema umeme uliopo haukidhi mahitaji ya matumizi yake ambapo asilimia kubwa ya wateja wake wanapatikana majira ya jioni muda ambao hawaruhusiwi kutumia umeme kwa kuwa umeme unaoanza kutolewa jioni ni wa genereta ambao hutolewa kwa matumizi ya nyumbani tu na sio kwa ajili ya viwandani vidogovidogo.

“ Majira ya saa tatu asubuhi ndio umeme unawashwa na ikifika saa kumi na moja jioni tunazuiliwa kuendelea na kazi wakati ambao ndio wateja wangu wanakuwa wanahitaji huduma ya kuchomelea mara baada ya wao kutoka mashambani na ndio muda ambao siruhusiwi kuendelea na kazi jambo hili linaniadhiri sana kiutendaji na kuona kuwa umeme huu hauna faida katika kazi yangu”

Maafisa wa REA na EWURA wakizungumza na wajasiriamali katika kijiji cha Kagerankanda wanaolalamikia uhaba wa umeme wa uhakika, anayeongea ni mkurugenzi mkuu wa REA Hassan Saidy

Amesema huduma hiyo tangu ilipoanza mwaka 2019 imekuwa haitoshelezi mahitaji yetu, mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wa sola zenyewe ambapo hadi sasa mashine za kusaga na kukoboa bado zinatumia nishati ya mafuta ya taa na dizeli hali inayotudimiza kiuchumi.

Naye Yohana Kalonga pamoja na kuishukuru serikali kuwatoa kwenye matumizi ya koroboi na “vimoli”amesema gharama za umeme ni kubwa na kuwaomba wapunguze gharama kwa kiwango ambacho mwananchi wa hali ya chini anaweza kumudu kununua umeme lakini pia uwe na tija ya katika kuwainua kiuchumi badala ya kuwadidimiza.

Imani Kolonko naye amesema umeme huo kila inapofika saa tano za usiku huwa unazimwa na kulazimika kulala gizani hivyo wale ambao wanategemea kujiingizia kipato muda wa usiku bado inakuwa ni changamoto kwao hususani wale wanaoendesha vibanda vya video hasa wakati huu wa mpira wa kombe la Dunia lakini pia hata vijiji vya jirani vya Mvinza bado havina umeme lakini na wao wanahitaji kupata fursa hiyo licha ya kuwa na changamoto hizo.

Kwa upande wake Erick France, meneja

wa kanda ya magharibi kutoka kampuni ya Engie Power Corner amsema kutokana na mabadiliko ya bei yaliyoanza July 2020 yalichangia kwa asilimia 95 kwa wao kushindwa kutoa huduma bora ikiwemo kuwaunganisha wateja wapya.

France amesema kampuni iliendelea kupambana na changamoto hiyo ambapo hadi ilipofika April 2022 kampuni ilikuwa imeshajiimarisha na kuanza kutoa huduma bora kwa asilimia 90 ambapo malengo ni kuhakikisha huduma hiyo inafika sehemu za viwandani kwenye mashine za kusaga ili wananchi waweze kubangua mpunga na kukoboa mahindi kwa gharama nafuu kupitia huduma ya sola.

Akilizungumzia hilo mkurugenzi mkuu wa REA Tanzania Hassan Saidy amesema azma ya serikali ni kuhakikisha mishoni mwa mwaka ujao wa fedha 2023-2024 vijiji vyote 12,345 vinafikiwa na umeme na kwamba wataanza na mikoa michache na kisha Tanzania nzima

Hadi sasa mradi wa umeme katika kijiji cha Kagerankanda chenye wakazi 24300 na vitongoji vitano vya Mkamba, Katezi, Kagunga Nyanzaza na Katotwi wanufaika na umeme ambapo hadi sasa waliofikiwa ni 439, na aambao bado hawajanufaika ni wananchi 6785

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma