skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu

Jeshi la wananchi la Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa Vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili ambao wamemaliza mkataba wa miaka miwili wa mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kurudishwa majumbani.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Machi 9,2023 Jijini Dodoma Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda , amesema nafasi hizo zinawahusu vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha 4 na cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.

Luten Kanali Ilonda, amewataka wananchi kuwa makini na matapeli ambao hufanya utapeli pindi matangazo hayo ya nafasi ya kujiunga na Jeshi hili zinapotangazwa.

Vigezo vinavyozingatiwa wakati wa maombi wa nafasi hizo muombaji awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa ,Mwenye kitambulisho cha Taifa,Awe na afya nzuri na akili timamu,Awe na cheti halisi cha kuzaliwa,vyeti vya shule na vyeti  vya taaluma.
 
Imesisitizwa kuwa waombaji wote waandike maombi kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya Jeshi hilo Dodoma kwanzia leo tarehe 9,Machi hadi tarehe 20 Machi 2023 yakiwa na viambatanisho kama vile nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya nida, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya muombaji na maombi yanaweza kutumwa Kupitia njia ya barua pepe ulinzimagazine@tpdf.mil.tz

Wakati huo huo Jeshi la Kujenga Taifa JKT limewataka vijana wanaohitimu mafunzo ya kijeshi, kuacha tabia ya kuilalamikia Serikali kuhusu ajira, badala yake watumie stadi za maisha na ujuzi waliopatiwa vikosini, kuibua fursa za ajira binafsi ambazo zitawasaidia kukuza uchumi wao na Taifa.

Wito huo umetolewa katika kambi ya 821 KJ Bulombora iliyopo mkoani Kigoma, ambapo Mkuu wa Mafunzo na Oparesheni Jeshi la Wananchi, Brigedia Jenerali Charles Ndiege anatumia nafasi ya kuhitimisha mafunzo kwa kuwataka vijana kubuni shughuli za ujasiriamali ambazo zitakuwa ni ajira binafsi badala ya kusubiri Serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amewataka vijana waliohitimu mafunzo, kuwa wazalendo kwa Taifa na kutowadhuru raia wengine, wakati Kamanda Kikosi Luteni Kanali Juma Hongo akibainisha kuwa vijana wote kikosini wamepatiwa mafunzo ya stadi za maisha na kijeshi kwa ukamilifu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma