skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

Mfumo wa uuzaji wa mbolea za ruzuku kwa njia ya namba za usajili kwa mkulima na vibandiko maalumu kwa kila mfuko wa mbolea unaouzwa kwa bei pungufu ni moja kati ya mikakati iliyoanzishwa na serikali kwa lengo la kudhibiti uhujumu na utoroshaji wa pembejeo unaotajwa kuhujumu serikali kwa zaidi ya miaka 15.

Pamoja na mpango huo kuwa na lengo zuri la kuwasaidia wakulima kumudu gharama, bado zipo changamoto mkoani Kigoma zinazowakabili wakulima kwa namna wanavyopambana kupata mbolea hizo na namna serikali inavyoshughulikia malalamiko ya wakulima huku kukiwa na malalamiko ya utendaji mbaya kwa mawakala waliokabidhiwa dhamana hiyo.

Modesta Sakoma kutoka wilayani Uvinza ni mmoja kati ya wananchi wanaolalamika na kuiomba serikali kufikiria upya na kurudisha mfumo wa zamani ili waweze kupata mbolea kwenye maduka ya pembejeo tofauti na ilivyo kwa mawakala ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na kupoteza muda wakifuatilia mbolea hizo.

“Mimi nahisi mawakala wanahusika kwenye kuleta hizi changamoto kwakuwa ndio wanaotuyumbisha, kila siku wanataarifa mpya na mbolea hazipatikani kwa wakati, watu mpaka wanataka kupigana kwasababu ya utaratibu mbovu uliopo,huenda serikalini mfumo upo vizuri ila huku chini kuna konakona sana ni bora serikali ifikirie kuturejeshea mfumo wa zamani” Alisema Sakoma

Profesa Joyce Ndalichako (MB) Waziri ofisi ya waziri mkuu, kajira ajira na wenye Ulemavu (wa pili kushoto) akizindua uuzaji wa mbolea ya Ruzuku mkoani Kigoma (August 2022)

Naye Laban Paul kutoka kijiji cha Luchugi wilayani Uvinza ameiomba serikali kufanya utaratibu wa kuweka wakala wa mbolea kwa kila kata ili kuepusha gharama za maisha wanapoifuata mbolea manispaa ya Kigoma Ujiji

“Nilikuja kuandikishwa wiki iliyopita, nikapata namba ya kuchukua mbolea tarehe 17 Disemba, nina wiki sasa mjini nikisubiri tarehe ifike na foleni bado ni ndefu, huku nipo natumia pesa na mahindi yangu shambani yanaharibika, ni bora mawakala wasogezwe zaidi kwa wakulima vijijini na si wakae mjini, tunapata hasara nyingi” Alisema Paul

Akizingumzia changamoto hizo afisa kilimo wa mkoa wa Kigoma James Peter alisema ukosefu wa mitaji ya kutosha kwa mawakala wa mbolea waliosajiliwa na mamlaka ya mbolea nchini ni miongoni mwa sababu zilizosababisha changamoto ya upatikanji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima kwa wakati.

Alisema mkoa wa Kigoma ulipata mawakala 120 waliosajiliwa na mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania kwaajili ya kutoa huduma hizo ila kutokana na changamoto za mitaji wachache walijitokeza kutoa huduma hali iliyosababisha kero kwa wakulima kwa kufuata mbolea mbali na kuleta msongamano mkubwa

Profesa Joyce Ndalichako akimkabidi mmoja wa wakulima mfuko wa mbolea uliouzwa kwa mfumo wa ruzuku ya serikali alipotembelea na kukagua uuzaji wa mbolea kwenye ghala la ETG mjini Kasulu. Alihimiza uwajibikaji, uadilifu na kujali wakulima

“Wakulima kutoka halmashauri za wilaya za Uvinza, Buhigwe, Kigoma na baadhi wakitoka Kasulu hufuata mbolea Kigoma manispaa, ambapo kuna mawakala wawili tu kutoka kampuni ya YALA na ETG na hivyo kufanya uhitaji kuwa mkubwa kuliko uwezo wa mawakala hao jambo linalosababisha msongamano na kushindwa kuhudumiwa kwa wakati” alisema Peter

Alisema serikali kupitia wakala wa udhibiti wa mbolea imeweza kukabiliana na hali hiyo kwa kuongeza sehemu za kutoa huduma na kutoa maelekezo kwa kila halmashauri kuainisha maeneo ambayo wanadhani serikali inaweza kupeleka kampuni na wakala wenye nguvu ya kutoa huduma ili kupunguza adha ya namna ya upatikanaji wa mbolea na kwamba maelekezo hayo yanaendelea kufanyiwa kazi

Kwa upande wa wakala wa usambazaji wa mbolea kutoka kampuni ya ETG, Donard Burton alisema ukosefu wa mbolea kwa wakulima umetokana na wao kujitokeza kwa idadi kubwa zaidi ya waliojisajili kupata mbolea hizo na kwamba mpaka sasa baadhi ya mbolea kama za CAN na UREA za kg 50 zimeisha

Burton amefafanua kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa wakulima baadhi ilibidi waweke utaratibu mpya ambao mkulima akiandikishwa leo anachukua kesho na kwamba wangekuwa wachache wangeweza kuandikishwa na kuchukua mbolea siku hiyo hiyo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma