skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Wananchi wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera wametakiwa kushirikiana na mashirika ya Serikali na yasiyo yakiserikali katika kutoa taarifa sahihi za kupinga vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya wanajamii wilayani humo.

Akizungumza na kituo cha Buha Radio Meneja mradi wa PACT kizazi kipya kupitia shirika la Humuliza lililopo kata ya Nshamba wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera Bi. Lightness Mpunga alisema kuwa vitendo vya ukatili vimekuwa vikitokea kwenye maeneo mbalimbali  licha ya wao kwa sasa wameendelea kutoa elimu ya kutosha inayohusu masuala ya kupinga vitendo vya ukatili kwa wananchi ndani ya wilaya hiyo.

Bi. Lightness alisema kuwa katika kuhakikisha  vitendo vya ukatili vinakomeshwa ndani ya wilaya hiyo, kwa sasa wao kwa kushirikiana na shirika la Humuliza wameanzisha mradi wa ufundi wa ushonaji na vijana wa kiume ufundi selemala ili kuwajengea uwezo  wa kujitegemea na kuondokana na matendo mabaya ya makundi Rika yanayowapelekea vijana wengi kutotimiza ndoto zao .

“Kwakweli kwa sasa tumefanikiwa kwa kiasi fulani japo siyo kwa asilimia miamoja katika kuyafikia makundi mengi hasa ya vijana wote kwenye jamii kwa wilaya hii ya Muleba.Tumeendelea kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wa shule ikiwemo begi za kubebea daftari, kalamu,sare za shule, Daftari pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa watoto wa kike hasa pedi za kujisitili wakati wa enzi” alisema Lightness

Katika hatua nyingine meneja mradi huyo aliongeza kwa kusema kuwa shirika la Humuliza limeendelea kutoa elimu kubwa kwa jamii mbalimbali kwa kushirikiana na serikali ya wilaya ya Muleba siyo tu katika kupinga vitendo vya ukatili lakini hata kutoa msaada wa kisaikolojia,elimu ya kujikinga na maambukiza ya virusi vya ukimwi na ukimwi wenyewe na magonjwa mengine mengi.

Sisi kama shirika kwa wakati wote tunaendelea kutoa elimu ya maradhi mbalimbali ikiwemo ukimwi,magonjwa ya zinaa lakini pia elimu hii  haikuwaacha nyuma watoto wa kike kutambua namna ya kujiepusha  kubeba mimba za utotoni pamoja na ndoa kabla ya wakati.Naishukuru serikali yetu ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa mashirika ya kijamii katika kuhakikisha ukatili unakomeshwa” alisema  

Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Muleba Bw. Barnabas Richard aliwahasa wananchi wote wilayani humo kujiepusha na vitendo vinavyopelekea kutokea kwa ukatili wa aina mbalimbali  ikiwemo ukatili wa kingono kwa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na ukatili  wa kimwili,kisaikolojia na kijinsia pamoja na aina nyingine za ukatili  kwani kufanya hivyo  ni kinyume cha sheria za nchi zilizopo.

“Ofisi ya ustawi wa jamii wilaya ya Muleba kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yaliyopo tutaendelea kupambana na watu wanaofanya ukatili ikiwemo kuwafikisha kwenye vyombo vyetu vya sheria na niwaombe tu wananchi waendelee kutoa ushirikiano wao kwetu katika kutoa taarifa sahihi kwa mamlaka husika ili kukomesha vitendo vya ukatili ndani ya wilaya yetu”.

Je! hali ya ukatili Tanzania imepungua?

Wakati hatua ya mapambano dhidi ya ukatili ukiendela kwa wilaya ya Muleba  mkoa wa Kagera  kwa mkoa wa Kigoma hali bado siyo nzuri kulingana na taarifa iliyotolewa na Kamati ya kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) mwaka 2020,ngazi ya Mkoa ikiongozwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Ndugu. Moses Msuluzya ikiwa na lengo la kukagua namna kamati za Halmashauri zinavyofanya kazi.

Kaimu Katibu Tawala huyo alisema kuwa Mkoa wa Kigoma bado unachangamoto ya Vitendo vya ukatili vinavyofanyika kutoripotiwa na badala yake  kusuluhishwa ndani ya Jamii na familia hali inayofanya kuathirika kwa wahanga na jamii kukithiri kwa vitendo hivyo. Katibu Tawala huyo aliitaka Kamati hiyo kuibua mbinu mpya kwa kuendelea kutoa elimu ndani ya jamii katika maeneo ambayo vitendo hivyo vya ukatili vimekithiri na kutoa mawasiliano kwa maafisa Ustawi wa Jamii na Dawati la Jeshi la Polisi mkoani humo ili vitendo hivyo viripotiwe.

Hata hivyo; Licha ya kuwepo kwa juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kuhakikisha inatokomeza vitendo vya ukatili wa aina tofauti kama vile vitendo vya ulawiti, ubakaji na vingine vingi  kwenye  jamii lakini hali siyo ya kuridhisha  licha ya kuwepo kwa juhudi hizo. wananchi hawa wanasimulia hali ilivyo na athari za ustawi wa jamii yao. Sikiliza sauti hapa chini

Kwa mujibu wa Ripoti ya jeshi la polisi nchini Tanzania iliyotolewa mwaka 2021 inataja kuwa miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803 pekee, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini humo.

Ripoti hiyo pia ya jeshi la polisi nchini Tanzania inaonesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto mathalani kwenye ripoti hiyo kwa mwaka 2020 kiasi ya visa 7388 viliripotiwa kote nchini tofauti na mwaka 2015 ambapo matukio yapatayo  5,803 yaliripotiwa.

Huko jijini Mwanza mji uliopo mwambao wa kusini mwa ziwa Viktoria kaskazini magharibi mwa Tanzania vitendo vya ukatili viliripotiwa  pia kwa mwaka wa 2020 Karibu asilimia 61 ya wanawake wajasiriamali kwenye masoko ya Halmashauri ya jiji la Mwanza  na Manisipaa ya Ilemela walibainika kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutelekezwa na wenza wao wa kiume hali iliyopelekea wanawake hao kushindwa kumudu maisha yao kikamilifu.

Katika utafti uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanawake (kivulini) jijini Mwanza na kutolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Bw. Yassin Ally  kwa vyombo vya habari alisema kuwa wanawake  hao wanakabiliwa na changamoto  ya   kutafuta msaada wa kisheria  katika kuzifamu haki zao za msingi. Bw. Yassin aliongeza kwa kusema kuwa wazazi na walezi  bado wanao wajibu mkubwa  wa kutoa malezi bora kwa watoto  wao ili kutokomeza vitendo vya ukatili.

Hata hivyo licha ya kuendelea kuripotiwa vitendo hivyo vya ukatili bado Ulimwengu umekuwaukiadhimisha Siku ya Kupambana na Ukatili Dhidi ya Wanawake, ambapo kwa mwaka wa 2020 kaulimbiu yake ilisema  ”Ipake Dunia Rangi ya Chungwa: Nisikie Nami Pia. Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Inaanza na Mimi.” 

Katika ujumbe wake kwa siku hiyo ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alitoa wito mkubwa kwa jumuia ya kimataifa kuendelea kuchukua hatua madhubuti kwani ukatili huo ni changamoto ya haki za binaadamu duniani.

Ili kuhakikisha ukatili unakomeshwa katika jamii mbalimbali nchini Tanzania ni muhimu Serikali kupitia mamlaka zake zote kuendelea kutoa elimu juu ya athari zitokanazo na vitendo vya ukatili ndani ya jamii husika ili wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika vinapojitokeza viashiria vya ukatili. Vivyohivyo Taasisi za Serikali na Zisizo za kiserikali ziendelea kutenga bajeti zao za kutosha zitakazowezesha kutolewa kwa huduma mbalimbali na kwa haraka Zaidi .Kadha ikiwemo msaada wa kisheria kwa watu ambao wamepatwa na ukatili wa aina mbalimbali hali itakayosaidia kukuza mapambano kwa kuwa Tanzania bila ukatili inawezekana.

Imeandaliwa na Joel Daud

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma