skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Simiyu

Jamii wilayani Bariadi mkoani Simiyu kwa kushirikiana na jeshi la Polisi wamehimiza umuhimu wa usalama wakati wa sikukuu hususani kwa watoto na makazi yao

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Buha FM mjini Bariadi wananchi kadhaa wamekiri kuwepo kwa baadhi ya familia ambazo hazichukui tahadhari za kiusalama kwa watoto nyakati za sikukuu jambo ambalo ni la hatari kwa ustawi wa jamii na usalama wa watoto kwa ujumla

Shija Luhende ni baba wa watoto sita anasema mwaka 2000 aliwaruhusu watoto wakaenda kutembea siku ya sikukuu, kilichotokea mmoja aliyekuwa na umri wa miaka mitatu alipotea, hatua iliyopelekea kuanza kumtafuta usiku kucha.

“Mimi sitaki kabisa matembezi ya wanangu eti sikukuu, labda aende nao mama yao au mimi mwenyewe, yaani siwezi kusahau, huyu mmoja alipotea ndugu zake wanasema alibaki nyuma akiangalia ngongoti na wao walijua atakumbuka njia ya kurudi,cha ajabu yeye akafata kundi la watoto wengine. Tulikuja kumpata kesho yake kwa msamaria aliyekuwa kamhifadhi.” Alisema Luhende

Kwa upande wake Veronika Madirisha anaishauri jamii kutafuta njia mbadala za kuwapa furaha watoto nyakati za sikukuu akitaja kuwa yapo mambo yenye manufaa kwa familia tofauti na kuwaacha watoto kwenda mitaani au katika kumbi za starehe

“Unaweza kuwawekea mikanda mizuri ya kutoa elimu wakabaki nyumbani, mbona nayo ni sehemu ya kusherekea jamani, ya nini watoto kwenye makumbi barabarani tena cha ajabu wengi wao wanakuwa peke yao bila uangalizi hebu wazazi ,walezi tubadilike jamani” Veronika Madirisha makazi wa Izunya Bariadi.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda

Sehemu kubwa ya wazazi wanakiri kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanaposherekea kipindi cha sikukuu wawe wanajua wapo maeneo gani? wawe na mtu mzima lakini pia kuhakikisha wanarudishwa majumbani mapema, hasa hasa wale wadogo wa chini ya miaka nane kwenda chini.

Katika kuhakikisha watu hususan watoto wadogo wanakuwa salama msimu huu wa sikukuu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda amewataka wazazi na walezi kutowaacha watoto watembee peke yao kwani kipindi cha sikukuu wapo watu wanatumia vilevi kupitiliza na hali hiyo inaweza ikasababisha watoto kugongwa.

Aidha amewataka wananchi kusherekea kwa amani na utulivu huku akisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha sikukuu ya pasaka inasherekewa kwa amani na utulivu.

Tazama video hii kwa maelezo ya kina kuhusu mkakati wa Polisi kudhibiti uhalifu wakati wa sikukuu

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma