skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Felster Nestory Matinde – Buha FM Mwanza

Kufuatia kuipuka kwa ugonjwa wa polio nchini Malawi na kusababisha hofu kwa nchi za jirani, Serikali ya Tanzania imeazimia kuhakikisha Watoto chini ya umri wa miaka Mitano wanakupata chanjo ya polio ili kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Hayo yamebainishwa Leo jijini Mwanza na mganga Mkuu wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Dk Sebastian Pima wakati akitoa ufafanuzi wa maandalizi ya kampeni ya taifa ya chanjo kwa watoto wa miezi sifuri mpaka miezi hamsini na tisa.

Dk Pima amesema kuwa chanzo hiyo ya polio itasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa polio kama vile kupooza viungo, kusababisha ulemavu wa ghafla pamoja na ulegevu ambao umekuwa ukikatisha maisha ya watoto hali inayopelekea kupungua kwa idadi ya watoto.

“Chanjo hii ni mahususi kwa ajili ya kuwakinga watoto kutokana na mlipuko wa polio uliotokea nchini Malawi ambapo chanjo hii itaongeza Kinga dhidi ya ugonjwa wa polio” amesema Dk Pima.

Sambamba na hayo Pima ameiomba jamii ihamasike kuwapeleka Watoto wao katika vituo vya afya ili wapatiwe chanjo ya polio ambayo imekuwa ikitolewa na wizara ya afya.

Kwa upande wake meya wa jiji la Mwanza Sima Constantine amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika kampeni ya kudhibiti ugonjwa wa polio.

Wizara ya afya imekuwa ikitoa chanjo ya polio kwa miaka kadhaa iliyopita kwa lengo kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa polio.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma