skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Immaculate Makilika – WHMTH

Serikali imeendelea kusisitiza wananchi na taasisi kuhakiki taarifa zao za Anwani za Makazi nchini na kuwa taarifa hizo ni za msingi katika kutoa na kupokea huduma kwa kuhakikisha kuwa mawasiliano yote yakiwemo ya barua yanatumia Anwani za Makazi, fomu zote za kutolea na kupokelea huduma na Mifumo ya Huduma ya Kielektroniki inajumuisha kipengele cha Anwani za Makazi ikiwa ni pamoja na utambulisho wa aina yoyote.

Hayo yamesemwa jana (Januari 10, 2023) na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa redio TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi iliyopo mkoani Morogoro

“Baada ya Operesheni ya Anwani za Makazi mfumo upo tayari kutumika. Aidha, kabla ya kutumia wananchi na taasisi tunapaswa kuhakiki taarifa zetu za Anwani za Makazi zilizokusanywa na kuanza kutumia mfumo huu katika shughuli zote za kijamii na kiuchumi ili tupate manufaa tarajiwa”. Ameeleza Mhe. Naibu Waziri Kundo.

Aidha, amebainisha kuwa uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi unategemea eneo ambalo taasisi ama mwananchi alipo ama anapoishi. Pia, eneo linaweza kuwa lenye barabara ama mtaa au lisilo na barabara ama mtaa. Ambapo,
kwa maeneo yenye barabara ama mitaa, taasisi ama mwananchi anapaswa kujua nambari ya nyumba, jina la barabara na postikodi ambayo ni nambari maalumu ya kata.

Vilevile katika maeneo ambayo hayana barabara ama mitaa, taasisi ama mwananchi anapaswa kujua nambari ya nyumba, jina la kitongoji, jina la kijiji na postikodi.

Amefafanua  kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, viongozi na watendaji wanaombwa kuendelea kutoa elimu kwa umma hususan kuwafahamisha na kuwaelewesha Anwani zao za Makazi sambamba na namna bora ya kutumia Mfumo wa Kidigitali wa Anwani za Makazi (NaPA).

Aidha, Mhe. Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa ni vyema uratibu wa utekelezaji na matumizi ya mfumo uimarishwe katika ngazi ya halmashauri. Vilevile, wakusanya taarifa waliotumika katika kukusanya taarifa wakati wa operesheni ni vyema waendelee kutambuliwa na kutumika katika kusaidia wananchi wanapopata changamoto za anwani katika maeneo yao.

“Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni endelevu kwa sababu makazi yanaendelea kuongezeka, nyumba zinaendelea kujengwa na watu ama ofisi huendelea kubadilisha makazi ama kuhama. Hivyo, mnaombwa kuendelea kuweka jitihada za uendelezaji wa mfumo kwa kuweka miundombinu, kukusanya taarifa na kusahihisha taarifa”. Amesisitiza Naibu Waziri Mhe. Mhandisi Kundo.

Mwisho

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma