Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kama ifuatavyo:…
Na Anita Balingilaki, Simiyu
Mkoa wa Simiyu unatarajia kutoa chanjo ya polio kwa watoto 869,040 kwenye halmashauri zake zote sita katika awamu ya nne itakayoanza Desemba mosi hadi nne 2022.
Hayo yamesemwa kwenye kikao cha kamati ya afya ya msingi ya mkoa na mratibu wa chanjo mkoani hapo Bi. Beatrice Kapufi akisisitiza kuwa dawa za chanjo zimeshagawiwa na wanaendelea na kampeni ya kutoa elimu ili kuongeza uelewa kwa jamii na kuwafikia watoto wengi zaidi.
” Hii hapa ni awamu ya nne tayari dawa zilizogawiwa ni 890,000 na tunatarajia kuwa na timu 1668 ambazo zitafanya zoezi hilo” amesema Kapufi.
Awali mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda amemtaka mganga mkuu wa mkoa huo kuweka makadirio ya juu ya watoto wanaotarajiwa kupata chanjo ili kuwafikia watoto wengi zaidi huku akiwaasa viongozi wa dini kuwa sehemu ya kuwahamasisha waamini wao ili wajitokeze kuwapeleka watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata chanjo hiyo.
Aidha Dkt Nawanda amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha wanatoa chanjo zote kwa watoto ambao wanahitajika huku akiongeza kuwa zoezi hilo la utoaji wa chanjo litatekelezwa kwa asilimia 100 kwasababu kila kitu tayari kipo na kinachosubiriwa ni muda wa kuanza utekelezaji.

” Nitoe rai kwa RMO basi tujipangie malengo yaliyo makubwa zaidi… lakini naamini safari hii tumeweka maksio makubwa ili mwisho wa siku inatupa nafasi na sisi ya kuweza kuwafikia walengwa walio wengi zaidi …rai nyingine kwetu sisi tuliohudhuria kikao hiki tukawe mabalozi wazuri katika zoezi hili ” amesema Dkt Nawanda na kuongeza kuwa:
” Ndugu zangu viongozi wa dini kuanzia Ijumaa,Jumamosi na Jumapili katika ibada zetu basi tukaweke msisitizo zaidi ili tuhakikishe wanajamii wanafahamu …kila kaya kuhakikisha kuwa hakuna mtoto aliye chini ya miaka mitano ambaye hajapata chanjo tuhakikishe wote wanapata…wadau wote hakikisheni mnashiriki kikamilifu ” ameongeza Dkt Nawanda.
Mbali na hayo Dkt Nawanda amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji mkoani hapo kuhakikisha elimu hii inafika hadi ngazi za kaya huku akiongeza kuwa mkoa huo una lengo la kufikisha zaidi ya asilimia 100 ya uchanjaji.
Katika hatua nyingine mganga mkuu wa mkoa huo Dkt Boniphace Marwa amesema idadi ya watu waliopata chanjo ya UVIKO 19 imeongezeka na kuuwezesha mkoa huo kupanda kutoka nafasi ya tatu kutoka mwishoni hadi nafasi ya tano kitaifa( kumi bora kitaifa).
” Katika kipindi cha Agosti – Septemba tulikuwa nafasi ya tatu kutoka mwisho kwasababu hapa katikati kidogo hatukuwa na kampeni kutokana na ukosefu wa rasilimali mbalimbali…lakini tulipata wadau wakatushika mkono na sasa hivi tupo nafasi ya tano kitaifa kwasasa tumepanda juu hatupo mwisho tena” amesema Dkt Marwa