skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Tayari eneo limepatikana,kinachosubiriwa ni kibali tu

Na Anita Balingilaki,Bariadi.

Mkoa wa Simiyu utapata uwekezaji wa aina yake kwenye elimu uliozingati matokeo, tafiti za kimataifa za Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) zinazoonyesha uwekezaji kuanzia miaka ya awali huwezesha watoto kufauli na baadaye kuwa na kipato bora wafikapo ukubwani, hivyo kuchangia ustawi wa mkoa na taifa.

Kupitia serikali na wananchi, mwekezaji kampuni ya kuchambua pamba ya Alliance ( Alliance Ginnery) iliyopo Kasoli wilayani Bariadi, mkoa inatarajia kujenga shule ya awali mpaka chuo kikuu na mara baada ya kukamilika ujenzi kampuni itakabidhi kwa serikali kwa ajili ya kuiendesha.

Boaz Ogolla, ni meneja mkuu wa kiwanda hicho amesema tayari wameshapata eneo lenye zaidi ya ukubwa wa ekari 100 na wananchi wameshalipwa fidia, na tayari wameshapisha eneo hilo kilichobaki ni kibali cha ujenzi kutoka serikalini.

👆Boaz Ogolla meneja wa kiwanda cha kuchambua pamba (Alliance Ginnery ) kilichopo Kasoli .

Kampuni ya Alliance Ginnery imekuja kuongeza nguvu kwenye eneo ambalo ni kipaumbele cha serikali kwani uwekezaji kwa watoto wadogo unaendana na maeneo makuu ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) ya mwaka 2021/22 hadi 2025/26, na kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 serikali ilianzisha madarasa ya awali yanayowaandaa watoto kuanza elimu ya msingi ( kuanza darasa la kwanza) katika shule zote za serikali nchini.

Katika mahojiano, Ogolla amesema, ” tumeona bado wananchi wana uhitaji wa elimu, hapa Simiyu, sidhani kama tuna chuo kikuu lakini tumeona ni kitu muhimu kwa maisha ya binadamu na tumeamua kufanya jambo tofauti kidogo, tumeweka mnyororo ambao unaweza kusaidia jamii ambapo mtoto anaanza awali mpaka chuo kikuu.”amesena Ogolla.

Ogolla amesema mwanzoni wataanza na elimu ya awali na wataendeleza mpaka darasa la saba, sekondari hadi chuo kikuu.

“Lengo letu ni kulea jamii ambayo inalelewa kutoka awali mpaka chuo kikuu ikiwa ndani ya shule hiyo na sio kwamba tunataka kufanya biashara, hapana ni kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwenye shule zingine ambazo tulizijenga na kukabidhi serikali na mpaka sasa serikali inaziendeleza vizuri, na hii pia baada ya kukamilika tutaikabidhi serikali ambayo itaendeleza kwa mujibu wa taratibu za kiserikali” amesema Ogolla

Aidha amesema furaha ya kiwanda hicho ni kuona jamii ambayo inakizinguka kiwanda hicho inapata elimu, afya nzuri huku akiongeza kuwa kiwanda kinaitegemea jamii hiyo katika kupata malighafi yake.

“Hawa watu walio wengi ndio wakulima wanaolima pamba na sisi tunapata malighafi, tunahitaji wakati wowote tuwe na jamii ambayo inaelewa, lakini pia sisi tunaendelea kutambua juhudi zao na mapenzi yao ya kutuwezesha kukaa hapa (kasoli) na pia kupata malighafi ambayo inawezesha kuendesha kiwanda chetu “amesema Ogolla.

Kwa mujibu wa Ogolla, mchakato wa ujenzi wa chuo hicho umeanza muda mrefu na sasa wamefikia hatua ya kusubiria kibali cha ujenzi.

“Zoezi la kujenga chuo tulianza tangu miaka saba iliyopita tulikuwa na wadau ambao tulijiunga nao, lakini ili wakafanye kazi kwa roho safi kunahitajika iundwe taasisi tofauti na taasisi ya Alliance Ginnery bali taasisi ambayo inajitegemea, tayari tumetuma maombi yetu kwa msajili wa taasisi, pindi tutakapopata cheti (kibali) ambacho kitaturuhusu kujenga shule hii tutajenga, na hadi sasa hivi wametupa matumaini kazi kubwa imekwishafanyika imebaki kidogo ili tupewe usajili na tuendelee kusaidia jamii kama tulivyokusudia” amesema Ogolla.

Masanja Sallu ni katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi amesema mwekezaji huyo ni mfano wa kuigwa huku akiongeza kuwa rai ya chama hicho ni vema wawekezaji wengine wilayani hapo wakaiga mfano huo kujitolea na kurudisha kwa jamii.

Eneo kitakapojengwa Chuo kikuu wilayani Bariadi mkoani Simiyu

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi Khalid Mbwana amesema wao ( Halmashauri) waliingia makubaliano rasmi ya kupata eneo toka kwa wananchi ambapo halmashauri hiyo ililipa fidia kwa wananchi na hivyo halmashauri kukabidhi eneo kwa mwekezaji.

Aidha Mbwana ameongeza kuwa halmashauri imeshiriki kwenye hatua zote za awali na kuwa bega kwa bega kuwasaidia kufanikisha jambo hilo.

Kwa mujibu wa afisa elimu mkoa wa Simiyu Mwl Majuto Njanga, amesema mkoa huo una jumla ya shule za msingi 592 miongoni mwake za serikali ni 578 na za binafsi ni 14, shule za sekondari zipo 168 ambapo za serikali ni 155, binafsi ni 13 huku zenye kidato cha tano zikiwa 13, shule 11 za serikali na mbili binafsi.

Kwa upande wao wananchi, wakiwemo wakazi wanaozunguka eneo linalotarajiwa kujengwa shule hiyo wamempongeza mwekezaji huyo ambapo wamesema ujio wa chuo hicho mbali na kuwawezesha watoto wao kupata elimu karibu pia kutafungua shughuli za kibiashara na hatimaye uchumi wa eneo hilo utakuwa kwa kasi kubwa na hivyo kuongeza mapato kwao, kwenye halmashauri na taifa kwa ujumla.

” Sisi tunafurahi kwa kweli hapa tunaweza kufungua maduka, hoteli tutajenga, nyumba za kupangisha kwaajili ya watumishi na pengine wanachuo kiukweli kwetu hii ni fursa tutapata kipato lakini na serikali itakusanya kodi” amesema Tabu Mlyambelele mkazi wa kasoli.

” Ujio wa shule hii ni neema kwetu kama mimi mama ntilie wakianza ujenzi ntawauzia mafundi chakula lakini na shule ikifunguliwa ntaendelea kuuza chakula,hali ikiwa nzuri ntatoa ajira kwa watakaokuwa wananisaidia kwani kwasasa ninao wawili tu maana biashara bado haijawa kubwa ila kikufunguliwa naamini biashara itakuwepo na pesa pia” amesema Tatu Maduhu mkazi wa Kasoli.

Kampuni hiyo imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwenye sekta mbalimbali mkoani Simiyu ikiwemo ujenzi wa zahanati, shule, chuo cha VETA, muindombinu ya elimu ikiwemo vyoo, madawati sambamba na uchimbaji wa visima virefu ambapo miradi yote hiyo imetumia kiasi cha bilioni 1,685,449,346 huku eneo pekee la ujenzi wa shule hiyo likinunuliwa kwa kiasi cha shilingi milioni 116 ikiwa ni sehemu ya kulipa fidia kwa wenye mashamba/maeneo yote ikiwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kufikisha huduma karibu na jamii.

Kukamilika kwa chuo hicho kutuwezesha mkoa wa Simiyu kupata chuo kikuu cha kwanza ambapo mpaka sasa mkoa huu una chuo kikuu huria na chuo cha fedha tawi la Sapiwi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma