skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika leo tarehe 29 Machi, 2022 umeipitisha nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa mwanachama mpya wa jumhia hiyo na kufanya idadi ya wanachama kufikia mataifa 7.

Kukubaliwa kwa DRC kuwa mwanachama kumefanyika baada ya mchakato mrefu wa kuyajadili maombi ya nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu na ukubwa kijiografia ambayo pia bado inakabiliwa na makundi ya waasi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Kufuatia maazimio hayo nimezungumza na wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walioko Tanzanina kuhusu umhimu wa nchi yao kuwa sehemu ya Afrika mashariki. Kwanza ni Fataki Bachinge kutoka Uvira akiwa katika kambi ya Nyarugusu nchini Tanzania, yeye anataja kuwa kujiunga kwa nchi yake katika jumuiya ya afrika mashariki kutafungua fursa Zaidi za kiuchumi na ushirikiano baina ya raia wa ukanda mzima

Kwa upande wake Gustavo Mekki anataja kuwa DRC kujiunga Afrika mashariki ni hatua sahihi na kwamba sasa Watoto na vijana walioko uhamishoni watakuwa na fursa ya masomo kwa mtaala wa DRC na pia kusoma masomo yanayoshabihiana ma nchi za Afrika mashariki ikiwemo kusoma kingereza toafauti na sasa ambako mfumo wa elimu wanaoipata Kambini haioneshi kuungwa mkono na vijana wengi

Tanzania imekuwa na mahusiano makubwa ya kikanda sambamba na unasaba wa watu wa pande zote mbili hususani ukanda wa ziwa Tanganyika ambalo huziunganisha nchi hizo, je watanzania wao wana maoni gani kuhusu hatua hiyo? Azizi Mnishi ni kiongozi wa chama cha wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda TCCIA mkoani Kigoma

“Niliposikia mapema leo asubuhi kuwa Marais wetu wameridhia DRC iwe mwanachama nimefurahi sana kwasababu sisi Tanzania pamoja na Congo, tuna mahusiano mazuri hasa kibiashara katika ukanda wetu wa Ziwa Tanganyika, kwahiyo kujiunga kwao kunaongeza chachu ya ushirikiano wa kiuchumi baina yetu” Anasema Azizi Munishi kiongozi wa TCCIA

Anasisitiza kuwa kwa sasa kusafiri kwenda DRC inahitajika kulipia Viz ana kwamba endapo watajiunga rasmi gharama hizo zitaondolewa au kupunguzwa na hivyo kuchochea ukuaji wa mahusiano ya ujirani mwema.

Kujiunga kwa DRC katika jumuiya ya Afrika mashariki kunaifanya kanda hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu wapatao milioni 555 kutoka watu milioni 465 wa awali na hivyo kuifanya kanda hiyo kuwa soko mhimu kwa mataifa yaliyoendelea baada ya kuwa na mfumo wa pamoja wa forodha.

Mwandishi: Prosper Kwigize

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma