skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Naibu balozi wa Burundi katika ubalozi mdogo wa Burundi mkoani Kigoma nchini Tanzania Bw. Adalbert Nininahazwe ameahidi kutoa ushirikiano kwa chama cha waandishi wa habari cha mkoa wa Kigoma KGPC katika kuhakikisha Tanzania na burundi zinapashana habari kwa kuzingatia weledii na maadili ya taaluma hiyo ili kuendeleza undugu na kusukuma kasi ya maendeleo baina ya nchi hizo mbili

Nininahazwe ametoa kauli hiyo mkoani Kigoma katika sherehe za siku ya uhuru wa vyombo vya habari ambazo katika mkoa wa Kigoma zilifanyika Mei 16 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa habari, viongozi wa serikali na vyombo vya dola wakiongozwa na mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye

Balozi Nininahazwe alibainisha kuwa, Burundi na Tanzania ni ndugu na pande zote zinapaswa kupashana habari ili kuwasaidia wananchi wa pande hizo kupata taarifa sahihi, na ameahidi kuwa serikali ya Burundi itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na kuwapa ushirikiano wa waandishi wa habari wa mkoa wa Kigoma ambao una unasaba mkubwa na nchi ya Burundi kijamii, kiusalama, kiuchumi na kiutamaduni.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, aliwataka viongozi na wadau wa habari  kushirikiana na waandishi wa habari kwa kuwapa nafasi ya kufanya kazi zao kwa uhuru badala ya kuwatumia kwa maslahi yao

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akihutubia waandishi wa habari na wadau mbalimbali wakati wa kilele cha siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma.

Alisema ni jambo baya kujenga urafiki ambao utawafanya waandishi wa habari kuandika mambo ambayo yatawafurahisha viongozi badala ya kuikomboa jamii

“Ni vizuri vyombo vya habari vikaandika habari kwa uhuru kwa maana ya kukosoa, kuelimisha na kuuitaarifu jamii mambo yanayotokea lakini jambo hilo linapaswa kufanywa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na taratibi zinazoongoza sheria na taratibu za  uandishi na kwamba viongozi na wadau wanapswa kujibu na kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali badala ya kuandika habari za upande mmoja ambazo nyingine zinazua taharuki kwenye jamii,” Amesema Andengenye

Pamoja na hivyo alisema kuwa mkoa wa Kigoma unafunguka kwenye suala zima la masuala ya uchumi hivyo ni vizuri vyombo vya habari vikatumika kutangaza rasilimali za mkoa na viongozo wa serikali, taasisi za umma na wadau wa habari wanapaswa kutoa taarifa bila kificho  kwaajili ya ustawi wa mkoa

Kwa upande wa Rais wa umoja wa vyama vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) ambae pia ni mwenyekiti wa club ya waandishi wa habari mkoani humo Deogratius Nsokolo aliweka bayana kuwa tayari mazungumzo baina ya viongozi wa chama cha waandishi wa habari cha Burundi zimeanza ili kuunganisha nguvu kwa kubadilishana ujuzi, uzoefu na habari kutoka pande zote mbili.

Nsokolo aliweka bayana kuwa tayari mazungumzo baina ya Kigoma na mkoa wa Makamba nchini burundi yameanza na kiongozi wa waandishi wa habari wa mkoa wa makamba Bw. Joel Buchumi ameonesha nia ya kuanzisha ushirikiano maalumu na Tanzania

Na katika hatua nyingine, Bw. Nsokolo amesema  kuwa viongozi wote wa serikali ya ya mkoa na taasisi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wanahabari pale  wanapohitajika kufanya hivyo hali itakayosaidia kuutangaza  mkoa na fursa zilizopo

“Niwaombe wadau wetu wa habari kutumia vyombo vya habari vilivyopo Mkoani kwetu kutangaza mazuri na fursa mbalimbali siyo hadi tusubiri ziara za viongozi wa Kitaifa” Alisema Nsokolo

Siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 3 kila mwaka, na kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ni uandishi wa habari na changamoto za kidijitali.  

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma