skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane-Kigoma

MAKAMU wa Raisi Dk.Philip Mpango amezitaka taasisi za kibenki nchini kupeleka  huduma zao vijijini  kutokana na mahitaji makubwa ya huduma katika maeneo hayo.

Amesema hayo jana wilayani Buhigwe mkoani Kigoma alipokuwa akifungua tawi la benki ya NMB wilayani humo na kusema kuwa ni muhimu benki  kupeleka huduma vijijini kwenye maeneo yanayokidhi vigezo kwani vijiji vingi vinahitaji uwepo wa  huduma za kibenki.

Amesema, yapo maeneo ambayo wananchi wanatembea kwa umbali mrefu kufuata huduma za kibenki akitoa mfano wa kijiji cha Kilelema wilayani humo ambao iliwalazimu kutembea kilometa 72 na kijiji cha Janda walitembea kilometa 95 kufuata huduma za benki wilayani Kasulu hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hivyo kusababisha wananchi wengi kuhifadhi fedha zao ndani kwenye mitungi.

Makamu wa Raisi Dk.Philip Mpango (katikati) akikata utepe kuzindua tawil la Benki ya NMB wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kushoto ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB Edwin Mhede

“Pamoja na maendeleo ya kiteknolojia yanayofanywa na mitandao ya simu kutumika pamoja na mawakala wa benki kwa lengo la kutoa na kupokea pesa bado kuna umuhimu  mkubwa wa kuwa na huduma za kibenki karibu kwani zinahitajika sana” Amesema Mpango.

Makamu wa Raisi amesema kuzinduliwa kwa tawi la NMB Buhigwe  kuna maana kubwa katika mchakato mzima wa maendeleo ikiwemo maendeleo  katika uwekezaji, utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na mikopo kwa wakulima na wafanyabiashara.

Tawi jipya la bank ya NMB Bugigwe mkoani Kigoma, Sasa NMB ina zaidi ya matawi 200 nchini nzima

Akizungumzia uzinduzi huo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB,Filbert Mponzi amesema kuwa benki hiyo imeweza kufikisha matawi 229 nchi nzima na mashine za kutolea fedha 180 huku ikiwa na mawakala zaidi ya 20,000 na tawi la Buhigwe lililofunguliwa leo linafanya mkoa Kigoma kuwa na matawi sita.

Mponzi amesema kuwa kufunguliwa kwa tawi hilo kunalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kwa tawi la Buhigwe benki imetenga shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kutoa mikopo na tawi hilo litakuwa na huduma zote za Kibenki kama matawi mengine nchini.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma