skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Shirika la OHIDE lenye lengo la kuinua kiwango cha upashanaji wa taarifa za maendeleo na uwekezaji mkoani Kigoma limefanikiwa kupewa kibali cha kuanzisha kituo cha Radio kiitwacho BUHA ambacho kitafanya kazi za kuhabarisha, kuburudhisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kilimo, mazingira na mahusiano bora kati ya wakimbizi na wenyeji katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA, BUHA FM RADIO imepewa masafa ya 100.1MHz Kasulu na taratibu za ukamilishaji wa ujenzi wa mfumo wa matangazo sambamba na majaribio umeanza.

Buha FM inatarajia kusikika katika mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani na itatoa huduma kwa kutumia mfumo shirikishi jamii katika kutambua mahitaji yamsikilizaji au jamii yenyewe badala ya mfumo unaotumiwa na radio nyingi nchini wa kuwalisha wananchi habari na elimu bila kujali kama habari na elimu inayotolewa kupitia vituo hivyo ina tija au lah

Mmoja wa waasisi wa Radio hiyo ambaye pia ni katibu mtendaji wa shirika la OHIDE Bi. Silesi Malli amebainisha kuwa, BUHA ni jina la heshima linalomaanisha watu wa Kigoma na mkoa wa Kigoma hivyo utendaji wa kituo hicho utazingatia sana TUNU za mkoa wa kigoma na nchi ya Tanzania ili maudhui yatakayozalishwa na kurushwa yalete mabadiliko chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Bi. Silesi Malli (kulia) akisalimiana na mwenyekiti wa kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu alipotembelea kambi hiyo kutambulisha mpango wa kuwa na radio shirikishi jamii kwa ajili ya watanzania na wakimbizi.

Bi. Silesi ambaye pia ni mwenyekiti wa Asasi ya Umoja wa mataifa nchini Tanzania (UNA) amesema jamii za vijijini hasa mikoa ya pembezoni imekuwa na ombwe kubwa la uhaba wa fursa za utoaji na upatikanaji wa habari za maendeleo jamboo linalopelekea kuendelea kubaki nyuma kiuchumi na hata kiusalama.

Amesisitiza kuwa OHIDE kupitia Buha FM itashirikiana na serikali bega kwa bega pamoja na mashirika mengiine ya kijamii na ya kimataifa yanayotoa huduma kwa wakimbizi kuelimisha umma juu ya fursa mbalimbali za kimaendeleo sambamba na utatuzi wa migogoro baina ya jamii yenyewe na baina ya Wakimbizi na wenyeji.

“Kasulu imekuwa nyuma katika uwanda wa mawasiliano licha ya kuwa ni mji pekee nchini Tanzania unaokua kwa haraka zaidi na kwa nguvu za wananchi wenyewe ukilinganisha na miji mingi nchini Tanzania licha ya kukabiriwa na changamoto nyingi za miundombinu za usafiri na usafirishaji, Radioo hii itasaidia kupaza sauti za wananchi.” Anasisitiza mmoja wa viongozi wa OHIDE ndugu John Biduga.

Buha FM itaanza kurusha rasimi vipindi hivi karibuni baada ya taratibu za ujenzi kukamilika.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma