skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maktaba Mtandao ili kuongeza wigo wa upatikanaji huduma za maktaba kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji wa huduma hiyo nchini.

Hayo yamesemwa leo Januari 3, 2022 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (Mb) wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA) ambapo amesema fedha hizo ni sehemu ya Shilingi bilioni 10.5 za bajeti ya maendeleo ya Bodi hiyo zilizotolewa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, Dkt. Mboni Ruzegea wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania. Uzinduzi wa Bodi hiyo umefanyika Januari 3, 2022 Jijini Dar wa Salaam.

Aidha ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha katika utafutaji wa machapisho na vitabu izingatie kupata vitabu vinavyolenga kukuza ujuzi, maarifa na stadi mbalimbali kwa Watanzania wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.

“Nitoe rai kwa Bodi kuhakikisha mnatafuta machapisho na vitabu vinavyolenga kukuza ujuzi, maarifa na stadi mbalimbali. Tunataka maktaba iwe kwa Watanzania wote yaani watoto, wajasiriamali, walemavu wa aina mbalimbali, wakulima, wafugaji, watafiti wote waweze kupata huduma hii muhimu,” amesisitiza Waziri Ndalichako.

Imeandikwa na mwandishi wetu, Dodoma

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma