skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Adela Madyane

Mamlaka ya bandari (TPA) mkoani Kigoma imeendelea kufanya maboresho kwa kuongeza vifaa vya kisasa vya kupakia na kupakua shehena ili kuongeza tija na ufanisi wa bandari  na kuongeza kipato katika pato la taifa.

Akiongea na waandishi wa habari katika bandari ndogo ya Kibirizi meneja wa bandari za ziwa Tanganyika Edward Mabula amesema kuwa maboresho hayo yameifanya bandari ya Kigoma kuwa na mafanikio makubwa katika kuongeza usafirishaji wa shehena kwenda na kutoka kwenye nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Mabula amevitaja baadhi ya  vifaa vilivyonunuliwa kuboresha miundombinu kuwa ni pamoja mashine tisa za kushusha na kupakua shehena (Folk Lifty, winchi za kuvutwa na gari (Mobile crane) na trekta zenye winch ambazo zote zinarahisisha usafirishaji wa shehena.

Amesema kwa mwezi bandari ya Kigoma  inasafirisha wastani wa tani laki tano na inakusanya wastani wa shilingi milioni 500 na kwamba imekuwa na mchango mkubwa katika kuifungua bandari ya Dar es Saalam kwani shehena kubwa inayopitia bandari ya Dar es salaam inaenda nchi ambazo zipo kwenye ziwa Tanganyika hususan Congo DRC ambayo huagiza shehena kwa asilimia 83.

Moja ya mitambo mipya inayotumika katika bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika nchini Tanzania

Kwa upande wa ukarabati wa bandari za Kigoma, Mabula amesema kuwa serikali inatarajia kuanza kufanya ukarabati kwenye eneo la jengo la abiria na njia za kuingilia bandarini chini ya ufadhili wa JAICA kuanzia mwezi Septemba kwa kipindi cha miezi sita utakaogharimu dola milioni 21.

Tito Francis mfanyabiashara na msafirishaji wa chumvi na juisi kuelekea nchini Congo alisema mamlaka ya bandari pia imeanza kufanya ukarabati  wa miundombinu ambayo ilikuwa inaleta changamoto za usafirishaji wa mizigo kwa wakati na kwamba kwa sasa anaweza kufanya shughuli zake bila kipingamizi huku changamoto kubwa kuwa uchache wa mabehewa.

Kwa upande wa wakala wa usafirishaji wa shehena Julienne Mutabihirima ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Shegema iliyopo bandari ya Kibirizi alisema kutokana na kuboresha miundombinu ya ushushaji wa shehena sasa wanashusha tani 400 kwa masaa matatu jambo ambalo lilikuwa gumu miaka miwili iliyopita ambapo walishusha shehena za ujazo huo huo kwa siku tano.

Mbaraka Said ambaye ni wakala wa meli za kusafirisha shehena alisema vifaa vya kisasa vilivyopo vimesaidia kushusha na kupakia mizigo kwa wakati na kwamba sasa mizigo inadhibitiwa tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita na kuiomba serikali kuboresha usafiri wa reli ili kupunguza gharama zinazotumika kusafirisha mizigo kutumia barabara kutoka mkoani Kigoma kuelekeza nchi za Congo, Burundi na Zambia.

Akizungumzia changamoto ya mabehewa mkuu wa kituo cha reli Kigoma Ally Shamte alisema serikali ipo kwenye mpango wa kukarabati mabehewa 600 kwa ajili ya kuja kuondoa changamoto iliyopo na kuboesha uchumi wa wafanyabiashara

Sikiliza maelezo ya Meneja wa kituo kikuu cha Gari moshi mjini Kigoma Bw. Ali Shamte
Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma