skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Bariadi.

Askari wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu mwenye no H.4178 PC Abati Benedicto Nkalango (27) aliyempiga mwanae ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kesi hiyo namba 8 ya mwaka 2023 inayomkabili askari huyo imetajwa jana February 16, 2023 katika mahakama ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Bariadi Mariam Nyangisi.

Mwendesha mashtaka wa serikali Daniel Masambu aaliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa anashtakiwa kwa kosa moja la kufanya ukatili dhidi ya mtoto ambaye alikuwa chini ya malezi yake.

Masambu amesema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 169(A) kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022.

Mtoto aliyejeruhiwa vibaya na baba mzazi kwa kile kinachotajwa kuwa alishindwa kusoma na kuandika

Libainisha kuwa Januari 15, 2023 mtuhumiwa alitenda ukatili kwa mtoto wake ambaye jina linahifadhiwa kwa kumchapa sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia majeraha madogo na makubwa sehemu za mgongoni na masikioni.

Mara baada ya kusomewa shitaka mtuhumiwa alikana na wakili wa serikali aliieleza mahakama kuwa upelelezi juu ya shauri hilo umekamilika na kuomba kutajiwa tarehe ya kuanza kusoma hoja za awali.

Kesi hiyo itaendelea tena March 2,2023 kwa hoja za awali ambapo hakimu wa mahakama ya wilaya ya Bariadi Mariam Nyangisi alimueleza mtuhumiwa kuwa dhamana ipo wazi.

Mtuhumiwa alishindwa kutimiza sharti la dhamana ambalo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho pamoja na bondi ya shilingi milioni 3 na hivyo kurejeshwa mahabusu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma