skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki ,Simiyu

Wazazi na walezi mkoani Simiyu, wametakiwa  kumpeleka  watoto Shule  ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa Mwaka wa masomo 2023.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala msaidizi anayeshughulikia elimu na mafunzo ya ufundi Mkoa wa Simiyu  ambaye pia ni  Afisa elimu mkoani humo,  Majuto Njanga wakati akizungumza katika kikao kazi cha mapitio ya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu Mkoa wa Simiyu.

Njanga alisema  Wanafunzi 32,814 katika wiki ya kwanza walioripoti ni Wanafunzi 7,272  sawa na asilimia 22.7 ya Wanafunzi wote waliochaguliwa.

“Kazi kubwa tunayofanya ni kuhamasisha  jamii kuhakikisha wanafunzi wote ambao wamechaguliwa wanafika  shule kwa muda unaotakiwa na tayari tumetoa taarifa kupitia vyombo vinavyohusika kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi, Serikali za kijiji na kata kuhakikisha watoto wanafika shule.

” Tunataka watoto wote pasiwe na changamoto itakayokuwa inamzuia…kama ni suala la sare za shule hana aende na zile za msingi wakati wazazi/ walezi wanaendelea kuwajibika kuwatafutia…tunatoa rai wale wote ambao wataonekana wanasita pasipo na sababu kuwapeleka watoto shule basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu  wa sheria ya elimu no 25 ya mwaka 1978 ambayo inasomeka katika sura 353 kifungu cha 35 @ 1 ambacho kinahitaji mwanafunzi aweze kuandikishwa katika masomo ambayo anaendelea nayo pasiwe na mtu ambaye anaweza kuzuia kuhakikisha anapata haki yake ya elimu,”  amesema Njanga.

Alisema suala hilo si kwa shule za Sekondari ni pamoja na watoto  ambao hawajaandikishwa elimu ya awali kwamba  wanatakiwa waweze kwenda shule na umri wa kwenda darasa la kwanza wapelekwe shule.

Washiriki wa kikao cha wadau wa Elimu mkoa wa Simiyu wakisikiliza maelezo ya afrisa elimu kuhusu mwitikio wa watoto wanaoanza kidato cha kwanza 2023

Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suzana Nyarubamba alisema Mkoa huo unatakiwa kuchukua hatua za madhubuti ili uweze kufanya vizuri kitaalam kwani kwa sasa umeshuka ambapo ametaka kupitia kikao hicho kutoa namna bora ya kutoka walipo na kusonga mbele.

Kwa upande, Paulina Nkwama ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)  alisema ni vema kuhakikisha wanafunzi  wanamaliza mzunguko ikiwa sambamba na kuhakikisha wanafunzi wanaoandikishwa kujiunga na elimu ya awali na darasa la kwanza ikiwa sambamba waliochaguliwa kujiunga  na kidato cha kwanza wanaripoti shule.

“Haya tusiyachukue kwa  wepesi, kati ya vitu vya msingi ambavyo tunapaswa kuvisisitiza ni  swala la uandikishaji wa elimu ya awali, darasa la kwanza na kuhakikisha  kidato cha kwanza wanaripoti… kingine tuhakikishe tunaondoa mdondoko wa wanafunzi, Kitaifa ni 0.8 iliyokuwepo mwanzo imepanda hadi 1.8 kwahiyo imeongezeka kwa kiwango kikubwa tunapaswa kuhakikisha wale wanaokuja shule wanakuwepo shule na tunawasimamia hadi wamalize  mzunguko.”

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya  Bariadi, Lupakisyo Kapange akiwataka wazazi wote wenye watoto wanaopaswa kwenda shule kuwapeleka shuleni mara moja.

“Mkoa huu (Simiyu) ni wa kichungaji wanaamini kwamba mtoto akienda kuchunga mifugo anakuwa amefanya tija ndani ya familia/ familia wanaamini kwamba wakiozesha mtoto wa kike ng’ombe 20 wanakuwa wamefaidika ndani ya jamii sasa sisi mkoa wa Simiyu hatukubaliani na hili Hakuna mwanafunzi ambaye hatohudhuria darasani wanafunzi wote waliofaulu wanatakiwa kuwa shule.Walimu wetu wana utayari wa kufanya kazi, Mheshimiwa  Rais ametujengea madarasa 239 mkoani kwetu, wote waliofaulu waende shule,” alisema Kapange.

Neema  Makundi ambaye ni Afisa Elimu Taluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa alisema wapo tayari kuyatekeleza yote waliyoagizwa kuyafanya katika kikao hicho.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma