skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki,Itilima

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Malimi Masunga,(24) mkazi wa kijiji cha Mwamugesha  ameshitakiwa kwenye  mahakama ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu   kwa  makosa  matatu kosa la  kwanza likiwa kutorosha binti chini ya miaka 16 bila ridhaa ya wazazi kinyume na kifungu cha 134 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura  ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 ,

Kosa la pili ni kubaka  kinyume na kifungu cha 130(1)(2)e na 131(1) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 na Kosa la tatu ni kushawishi kuoa mwanafunzi kinyume na kifungu cha 60A(4) cha sheria ya elimu sura ya 353 kama ilivyo fanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Awali mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilaya ya Itilima mkaguzi msaidizi wa polisi Jaston Mhule ameiambia mahakama  kuwa mnamo June14, 2023 katika gulio la kijiji cha Ikindilo lililopo  wilayani Itilima mshitakiwa alimtorosha binti huyo (jina linahifadhiwa) kwa nia ya kumuoa na kwenda nae kijiji cha Matale na baadae kijiji cha Mbiti wilayani  Bariadi ambako aliishi nae kama mke na mme  kwa siku 25 mpaka Julai 7, 2023 na badae alimpigia simu mzazi wa binti huyo (jina linahifadhiwa) kwa lengo la kumfahamisha nia ya kumuoa binti yake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza.

Mwendesha mashitaka aliiendelea kuiambia mahakama kuwa na baada ya kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho  kwake na kwa jamii kwani tukio hilo linamadhara makubwa kwa binti huyo kisaikolojia  pia matukio kama haya huacha kumbukumbu mbaya isiyo futika kirahisi katika maisha ya mhanga na amemsababishia mhanga kukosa maarifa na ujuzi  ukizingatia serikali inatenga fedha nyingi ili watoto wote wapate elimu kwa manuafaa yao na taifa.

Julai 8, 2023 mshitakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Itilima na Agosti 7, 2023 hukumu ya shauri la jinai Na.34/2023 ilisomwa  katika mahakama ya wilaya ya Itilima mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya itilima Roberth Kaanwa na jumla ya mashahidi sita na vielelezo vitatu vilitolewa na upande wa mashtaka.na baada ya ushahidi huo mshtakiwa alijitetea  nakuita  mashahidi wawili upande wake na kuiomba  mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza .

Mahakama ya wilaya ya Itilima ilimtia hatiani mshitakiwa kwa makosa yote matatu .

ndipo hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya itilima Roberth Kaanwa akatoa hukumu, kosa la kwanza la kutorosha binti chini ya miaka 16 kwenda jela miaka 6, kosa la pili kubaka kwenda jela miaka 30 na kosa la tatu kushawishi kuoa mwanafunzi kwenda jela miaka 3 na adhabu zote zinakwenda kwa pamoja hivyo atatumikia miaka 30 jela.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma