skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Bariadi

Watoto watatu wamepoteza maisha huku wengine wawili wakinusurika kifo wilayani baada ya kusombwa na maji kwenye mto Pugu uliopo kijiji cha Pugu kata Itubukilo wilayani Bariadi

Tukio hilo lilitokea April 25 mwaka huu majira ya jioni wakati watoto hao wakizoa mchanga pembezoni mwa mto huo kwa ajili ya kuusafirisha kwenda kijijini kwenye shughuli za ujenzi ambapo mvua kuwa ilinyesha na maji yakaongezeka kwa kasi ghafla na kuwasomba na kusababisha kupoteza maisha

Kati ya watoto watatu waliofariki wawili ni kutoka familia moja ya Njile Malingisi, marehemu wametambulika kwa majina ya Malegi legi (16) mwanafunzi wa darasa la sita, Isaka Njile (14) mwanafunzi wa darasa la tatu na Wille Njile (8) mwanafuzi wa darasa la tatu wote walikuwa wanasoma shule ya msingi Itubukilo B iliyopo wilayani Bariadi.

Tukio jingine lilitokea April 29,2023 majira ya saa tisa na nusu alasiri ambapo watoto watano walizama kwenye dimbwi, na watatu kati yao waliopoteza maisha.

Tukio hilo limetokea kitongoji cha Mwabayanda, kijiji cha Ng’alita kata ya Matongo tarafa Dutwa wilayani Bariadi, ambapo watoto hao waliokuwa wanafua kando ya dimbwi lililochimbwa kwa ajili ya kupata Changarawe ya kutengenezea barabara walizama katika dimbwi hilo.

Kamanda wa kikosi cha Zima moto na ukoaji mkoa wa Simiyu Faustine Mtitu ameviambia vyombo vya habari kuwa dimbwi hilo lilikuwa limejaa maji na mtoto mmoja kati yao aliteleza wakati akijaribu kuchota maji ndipo wenzake wakadumbukia kumuokoa na katika harakati za kumuokoa wapo waliopoteza maisha.

Amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Martha Mbagule (17) mkulima, Jenipher Ng’habi (13) alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Ng’halita B darasa la sita na Tuma Luja (11) mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Ng’halita

Kufuatia tukio hilo, Serikali wilayani Bariadi mkoani Simiyu imepiga marufuku watoto kufanya kazi ambazo haziendani na umri wao ambapo miongoni mwa kazi hizo zipo ambazo zimesababisha vifo na nyingine kuhatarisha maendeleo na ustawi wa mtoto.

Marufuku hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya hiyo Simon Simalenga kwa nyakati tofauti akiwa kwenye mikutano ya hadhara ya kusikiliza kero za wananchi na kwa mara nyingine wakati akiongea na wakazi wa Itubukilo ambapo kulitokea vifo vya watoto watatu waliokuwa wakichota mchanga kwenye mto Pugu.

Miongoni mwa kazi zilizopigwa marufuku ni pamoja na watoto kuhusishwa kwenye zoezi la uchimbaji wa mchanga, na kuchunga mifugo ambapo baadhi ya wazazi /walezi wamekuwa na tabia ya kuwapa watoto wadogo kundi kubwa la mifugo ambayo kiumri hawaimudu na wengine kuchungia kando kando ya barabara.

Wananchi wakiwa pembezoni mwa eneo la tukio lililogharimu maisha ya watoto katika Mto Pugu wilayani Bariadi

Akiwa eneo la tukio mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga ametoa pole kwa familia na jamii ya Itubukilo huku akiwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuwa sehemu ya ulinzi dhidi ya matukio yanayoweza kuwadhuru.

Aprili 12, 2023 akitoa taarifa kwenye ufunguzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Simiyu SSP Namsemba Mwakatobe alisema baadhi ya changamoto zinazosababisha ajali mkoani hapo ni pamoja na wafugaji wakiwemo wazazi/walezi kuwatuma watoto wadogo kuchunga mifugo na kupelekea mifugo hiyo kuingia barabarani jambo linalohatarisha maisha ya watoto hao na mifugo waliyonayo.

“Mimi naona viongozi wa serikali wakikuta mtoto anachunga mifugo au kuchimba mchanga mzazi achukuliwe hatua mara moja akianza wa mfano hili litakoma unakuta mtoto mdogo ana kundi kubwa la ng’ombe jamani huu ni uonevu” Martha Seni.

“Sheria ichukue mkondo wake, sheria za watoto zifanye kazi, hawa ni taifa la kesho, sasa wakianza kufanya kazi ambazo hawaendani nazo tunawadumaza, majukumu makubwa kuliko umri wanapata wapi muda wa kucheza na wenzao pamoja na kujisomea” amesema Lucas Mitinje.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga (wa tatu kulia) akiwa na kamati ya ulinzi na usalama kwenye zoezi la uokoaji wa watoto waliosombwa na maji ya mto

Nao baadhi ya wananchi wa eneo ambapo tukio la vifo vya watoto vilitokea wamesema wamelipokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa.

“Tumepokea tukio hili kwa masikitiko makubwa baada ya kuzipata hizi taarifa, tunasikitika sana ni kwanini imekuwa hivyo watoto hawa walikuwa tegemezi kwa taifa la kesho tumelipokea kwa machungu mno” Mathias Pole

Inspekta Faustin Mtitu ni kaimu kamanda mkoa, jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Simiyu amethibitisha kutokea kwa vifo vya watoto ambapo amesema watoto watano walisombwa na maji ya mvua wakati wakichota mchanga na watatu kati yao walipoteza maisha.

“wakati wakiendelea na zoezi la kuchota mchanga mvua kubwa ilinyesha na maji yakawasomba, ni vema wananchi wakachukua tahadhari ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto/watoto wajue watoto wapo maeneo gani? je ni salama kwao?”amesema Inspekta Mtitu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu, matukio ya uokoaji yanayosababisha vifo vingi mkoani hapo ni matukio ya ajali za majini na kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka April 29 watu 10 wamekufa maji wakiwemo wanaume sita, wanawake watatu kati yao alikuwepo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Inspekta Mtitu amesema watu hao wamepoteza maisha kwa matukio tofauti huku akiwataka wananchi kuongeza umakini hususan kipindi hiki cha masika (mvua).

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma