skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Simiyu

Maji ni uhai lakini yanapotumika kinyume na matarajio au yasipo dhibitiwa, yanaweza kusababisha maafa na madhara makubwa kwa jamii hususan watoto wadogo.

Maji ambayo yanapatikana kwenye visima na madimbwi yanatajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya vifo vya watoto wadogo na watu wazima mkoani Simiyu ambapo Wilaya ya Bariadi inatajwa kuwa inaongoza kwa matukio hayo ambapo pia ina idadi kubwa ya visima na madimbwi.

Wapo wananchi ambao kabla ya kuunganishwa maji ya bomba walikuwa wanatumia maji ya visima na hata baada ya kupata maji huduma ya maji safi na salama (ya bomba) kuna muda hutumia maji ya visima kwa matumizi mbalimbali.

Kwa upande wa madimbwi jamii kubwa ni ya wafugaji ambao huyatumia kunyweshea mifugo yao hususan kipindi cha masika na hata kiangazi.

Baadhi ya visima sio rafiki kwa uhai wa binadamu kutoka na kutokuwa na mifuniko na hii hupelekea watoto wadogo na hata watu wazima kudumbukia na kuumia au hata kupoteza maisha.

Miongoni mwa madhara yaliyotokana na visima visivyofunikwa ni pamoja na kisa cha mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye alitumbukia kwenye kisima cha maji kilichopo nyumbani kwao na kupoteza maisha.

Jirani anasimulia

“Mama wa mtoto huyu alichota maji akasahau kurudisha mfuniko wakati akipeleka maji ndani, mtoto alikuwa anacheza hatua chache kutoka kisima kilipo, aliporudi hakumuona mtoto, alivyoaanza kumtafuta ndio akagundua katumbukia. Jeshi la zimamoto na uokoaji lilipata taarifa likafika,” Butondo Kwilasa.

Japokuwa elimu imekuwa ikitolewa mara kwa mara kupitia vyombo vya habari, na maeneo ya mikusanyiko bado baadhi ya jamii haitaki kubadilika.

Askari wa Jeshii la Zimamoto na uokoaji wakiopoa mwili wa mtu aliyepoteza maisha baada ya kuzama katika moja ya mito na mabwawa mkoani Simiyu hivi karibuni

“Matukio ya watu kutumbukia kwenye madimbwi,visimana mito si ya mara moja, elimu inatolewa lakini mabadiliko hakuna, sasa mtu umeambiwa fukia dimbwi na shimo au weka mfuniko kwenye kisima lakini hutaki, labda waanze msako wa kuwakamata wataelewa,” alisema Salome Mwandu.

“Kikubwa hapa sheria ichukue mkondo wake, ukaguzi ufanyike nyumba kwa nyumba wakikuta kisima kipo wazi, kamata piga faini! Inaweza kusaidia watu kubadilika” aliongeza Sayi Makoye

Taarifa kutoka kwa Kaimu Kamanda Mkoa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Simiyu, Inspekta Faustin Mtitu zinaonyesha kwa kipindi cha Januari hadi Februari 2023, jeshi hilo limepokea matukio 9.

Miongoni mwa matukio hayo matatu ni ya moto, sita ya uokozi na yamesababisha vifo vya watu wanne wakiwemo wakiume watatu na mwanamke mmoja. Kulikuwa na majeruhi wanne, wanaume watatu na mwanamke mmoja .

Matukio mengi yanayosababisha vifo mkoani Simiyu yametajwa kuwa yanatokana na visima, mashimo, madimbwi, mabwawa na mito ya msimu.

Afisa wa jeshi la zimamoto na uokoaji akitoa elimu ya udhibiti wa majanga na maafa kwa wananchi wilayani Bariadi

Jeshi hilo limewataka wananchi wote mkoani hapo kuchukua hatua na tahadhari zinazotakiwa.

Kuhusu hatua zitakazo chukuliwa na jeshi hilo ni kuanza kuvifungia visima vyote ambavyo havina uangalizi ili kudhibiti vifo vya watu wakiwemo watoto wadogo wa umri chini ya miaka mitano kuzama majini.

“Niwatake wananchi kuhakikisha visima vinafunikwa wakati wote wakati havitumiki, kuhakikisha mashimo yote ya vyoo ambayo ujenzi wake haujakamilika yanawekewa uzio, wazazi wasiwaruhusu watoto kucheza kwenye maeneo hatarishi ikiwa ni sambamba na kufukia madimbwi na mashimo ambayo hayatumiki,” Inspekta Mtitu alisema.

Inspekta Mtitu ameongeza kuwa, madimbwi ni mengi, uangalizi na usimamizi wa karibu umekuwa sio wa kuridhisha jambo ambalo linapelekea kutokea kwa ajali nyingi zinazogharimu maisha ya watu.

“Ili kukabiliana na changamoto hiyo tunaendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na hapa tunawafikia hadi wale wadogo kabisa, wananchi pia tumewafikia na tutaendelea kutoa kwenye mikutano ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa mpana wa hatari inayoambatana na visima au madimbwi ambayo wameyachimba kwenye maeneo yao kabla hatujaanza zoezi la kuvifungia,”amesema Inspekta Mtitu.

Awali, akiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji Marchi 22,2023 kilichofanyika kimkoa kata ya Ngulyati mkuu wa mkoa huo Dkt Yahaya Nawanda aliwata Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Simiyu wanapotekekeza miradi ya maji wahakikishe wanaweka maeneo ya kunyweshea mifugo, hatua hii itasaidia kupunguza uchimbaji wa madimbwi mara baada ya kukata mabomba.

Kwa mujibu wa meneja RUWASA mkoa wa Simiyu mhandisi Mariam Majala hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijijini mkoani hapo ni asilimia 71.

Ikumbukwe ulinzi na usalama wa mtoto ni jukumu la jamii kwa ujumla kwa mstakabili wa kesho yake iliyo njema, kuna umuhimu wa elimu kutolewa hadi kwenye vituo vya kulelea watoto mchana, madarasa ya awali mpaka la saba kwenye shule za msingi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma