skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

Taasisi ya Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na shirika la Kimarekani la Centres for Diseases Control (CDC) limefanikiwa kutekeleza mradi mahususi wa kufubaza virusi vya UKIMWI kwa asilimia 99 ya waathirika 25540 wanaoishi na maambukizi ya VVU mkoani Kigoma

Akitoa ya utekelezaji kwa robo ya mwisho ya Oktoba -Disemba 2022 katika ofisi za mkuu wa mkoa wakati wa matembezi ya kikazi ya mkurugenzi mkazi wa CDC katika maeneo ya mradi Dr Frederick Ndossi ambaye ni mkurugenzi wa Tiba na Matunzo wa mradi huo amesema mbinu mbalimbali zimetumika kuhakikisha matokeo hayo yanapatikana hussuan elimu endelevu, tiba, matunzo pamoja na ufuatiliaji.

Dr Frederick Ndossi Mkurugenzi wa Tiba na Matunzo kutoka THPS akitoa taarifa ya mradi wa afya hatua ofisini kwa mkuu wa Kigoma

Dr. Ndossi amesema kuwa ili kufikia mafanikio hayo taasisi ikishirikiana na serikali walihakikisha kila mgonjwa anayetumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi anakunywa kwa kufuata utaratibu mzuri na kila aliyepotea au kuacha kutumia dawa anatafutwa na kurudishwa kwenye matumizi sahihi na kwamba mpaka sasa wameweza kuhudumia na kufikia vituo vya tiba na matunzo 67 kati ya 83 kwa halmashauri zote za mkoa wa Kigoma. Aidha Ndossi amebainisha kuwa changamoto ni akina mama  wengi kutohudhuria kliniki ya baba, mama na mtoto pindi wanapojigundua kuwa wajawazito na kwamba wameweza kuwafikia kwa asilimia 16 huku jitihada mbalimbali zikifanyika kuwabaini ikiwemo kuongeza ufahamu wa akina mama hao juu ya umuhimu wa kliniki na kuhakikisha kila anayefika haondoki bila kufanyiwa vipimo.

kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dr. Jesca Leba amesema hadi sasa maambukizi ya UKIMWI yamepungua hadi kufikia asilimia 2.3   hali iliyotokana na mwamko wa jamii kupima na kuanza dawa mara moja kwa wanaogundulika kuwa na maambukizi sambamba na utoaji wa ushauri nasihi na matumizi sahihi ya dawa.

“Siku hizi hakuna taratibu ndefu, watu wametambua hali zao, mtu akipima akagundulika kuwa ana maambukizi anaanza dawa mara moja, tunapima uwingi wa virusi kwa wakati, tunafuatilia ufuasi mzuri wa dawa na tunapiga simu kwa wagonjwa wasiohudhuria vizuri kliniki kuhakikisha wanarudi, tunafanya uchunguzi kuhakikisha watoto wanaozaliwa  hawazaliwi na maambukizi, ni baadhi ya mbinu za kuzuia maambukizi sambamba na kuvifubaza virusi” Amesema Dr. Leba

Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dr. Leba akielezea namna walivyofanikisha utekelezaji wa mpango huo

Dr. Leba ameongeza kuwa, ili kuhakikisha akina mama wajawazito wanakwenda kliniki kupitia mradi wa “Afya Hatua”, wanaendelea kuhamasisha jamii kwa kutumia viongozi wa dini, watu maarufu, viongozi wa kimila na viongozi wa siasa ili kuhakikisha akina mama wanafika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara wanapojigundua ni wajawazito  na kisha kuendelea na uchunguzi mwingine na  wanaogundulika kuwa na maambukizi  kuanza dawa mapema sambamba na unasihi.

Kikosi kazi cha watoa huduma za afya wakiwa wanateta jambo, wa pili kulia (anayeongea) ni Dr Mahesh Swaminathan kutoka CDC , na kulia ni  Dr Robert Rwebangira  DMO wa wilaya ya Kasulu

Kwa upande wake Mkurugenzi mkazi wa CDC Mahesh Swaminathan ambaye almefanya ziara maalumu mkoani Kigoma, amesema lengo la matembezi hayo ni kuona namna fedha iliyotolewa imefanya kazi iliyokusudiwa, kuhimiza kufanya kazi kwa pamoja sambamba na kuongeza uwajibikaji na kwamba kwa Kigoma hilo limefanikiwa kwakuwa maisha ya watu yanaokolewa na hakuna pesa zinazopotea huku akiahidi kuwa taasisii yake itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali na wadau wengine katika mapambano dhidi ya virusii vya Ukimwi.

Naye mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema wanafurahishwa na  kazi inayofanywa na taasisi ya THPS kwakuwa wanajuhudi katika kuleta afya kwa wakazi wa mkoani humo kwa kutibu na kuzuia pale inapowezekana 

“Tunamuingiliano mkubwa wa watu kutoka nchi tunazopakana nazo hivyo maambukizi yanaweza kuwa rahisi kutokea, mkiendelea kufanya vizuri mtasaidia magonjwa yasiende kwenye nchi nyingine na hivyo kuufanya mkoa wetu kuwa salama” Amesema Andengenye

Timu ya afya mkoa kutoka THPs, CDC, na Ofisi ya RMO wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Kigoma baada ya kupata taarifa fupi ya ziara ya kikazi ya Dr Mahesh Swaminathan mkugenzi mkazi kutoka CDC.

Ameongeza kuwa THPS kupitia kampeni za chanjo ya Uviko 19 uliwezesha mkoa kutoka asilimia za tano za uchanjaji mnamo mwaka 2021 na kuongezeka mpaka kufikia asilimia 107 mwaka huu na kuufanya mkoa kuwa miongoni mwa mikoa vinara na kuwaomba kuendeleza ushirikiano ili watu wawe na afya njema na washiriki katika shughuli za kiuchumi.

Kwa taarifa zaidi kuhusu matukio mbalimbali ya THPS tafadhali tembelea tovuti yake kwa kubofya HAPA au ukurasa wake wa twitter kwa kubofya katika picha hapo chini

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma