skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwatumikia wananchi na kwamba ilani ya uchaguzi ya 2020 inatekelezwa.

“Chama kipo imara na kinaendelea kuwatumikia wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ambayo inatekelezwa kwa mafanikio makubwa, hivyo kila Mkuu wa Idara aone kilichoandikwa kuhusu eneo lake na atengeneze mpango kazi wa kuyatekeleza yaliyoahidiwa kwenye ilani hiyo.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 4, 2023) wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Miaka 46 ya CCM Mkoa wa Kigoma. Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika katika Uwanja wa Umoja wilayani Kasulu.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita, Mheshimiwa Rais Samia na Mwenyekiti wa CCM Taifa amefanikiwa kuboresha sekta mbalimbali zikiwemo uchumi, elimu, afya, maji, miundombinu, nishati, utalii pamoja na kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuwa kivutio cha wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali, ambapo amesema namna pekee ambayo Watanzania wanaweza kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na kuimarisha sekta hizo, Mheshimiwa Rais Samia anaendelea kuimarisha Muungano pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini ili waendelee kuwatumikia wananchi katika maeneo yote.

Awali, Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua ugawaji wa kadi za kielektroniki kwa mkoa wa Kigoma kwa kugawa kadi hizo kwa wanachama wapya 400 wa CCM wa wilaya ya Kasulu. Katika maadhimisho hayo Mkoa umefanikiwa kupata wananchama wapya 2,162 waliojiunga na Chama hicho.

Baadhi ya Viongozi na wanachama wakishiriki sherehe za miaka 46 ya CCM mkoani Kigoma yaliyofanyika mjini Kasulu

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma, Jamal Tamim alisema CCM imefanya mambo mengi tangu kuanzishwa kwake ikiwemo utoaji wa elimu ambapo awali elimu ya sekondari ilikuwa changamoto kwa watu wengi kutokana na uhaba wa madarasa licha ya kufaulu elimu ya msingi. “Kwa sasa shule ni nyingi ila nashangaa kwa nini wazazi hawapeleki watoto shule.”

Aidha ndugu Jamal amelaani vikali vitendo vya watumishi wa umma kuwahujumu wananchi badala ya kuwasaidia kutimiza malengo yake, huku akitolea mfano Mamlaka ya usimamizi wa Misitu TFS kupora mazao ya wakulima wanaobainika kulima katika hifadhi za misitu.

Mwenyekiti huo aliyechaguliwa mwaka 2022 ameitaka serikali kuwachukulia hatua watumishi wa Umma wasiotekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Mheshimiwa waziri Mkuu, tunakuomba utusaidie, hawa TFS wanakamata mazao ya wakulima, na haijulikani wapi wanayapeleka, na kama wanauza wanamuuzia nani na pesa walizouza watuoneshe Control Number tuone kama kweli hiyo pesa inaingia serikali au ni hujuma tu, wao wajibu wao ni kulinda misitu inakuwaje wanawaacha wakulima wanaingia, wanaanzisha mashamba, wanalima bila kuzuiliwa harafu wakivuna maafisa wananyang’anya mazao ya wakulima wetu, hii si sawa tunaomba serikali ichukue hatua” alisisitiza Ndugu Jamal Tamim

Naye, Mbunge Kasulu Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani na jimbo la Kasulu limefanikiwa kupata miradi mbalimbali ya elimu, afya, maji, barabara na kilimo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma