skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Prosper Kwigize na Adella Madyane

Serikali ya Tanzania kwa kututumia ufadhili wa serikali ya Uingereza imekusudia kuinua ubora wa elimu nchini kufuatia kubainika kuwepo kwa mapungufu makubwa yanayokwamisha ustawi wa elimu katika Nyanja mbalimbali

Akiongea katika kikao maalumu cha wadau wa elimu, wamiliki wa vyombo vya Habari na waandishi wa Habari mkoani Kigoma kilichofanyika leo mjini Kasulu, Mratibu wa mradi huo uliopewa jina la Shule Bora Bw. Celestine Mussa ameweka bayana kuwa maeneo yatakayotiliwa mkazo na mradi huo ni miundombinu, usalama, ufundishaji, ujifunzaji na ujumuishi wa Watoto wenye mahitaji maalumu.

Bw. Mussa amesisitiza kuwa mradi wa Shule bora unatarajia kutumia kiasi cha paundi za uingereza 89 milioni sawa na shilingi bilioni 271 ambazo zimetolewa na shirika la msaada la uingereza UK Aid na utatekelezwa hadi mwaka 2027.

“Tunatamani kuona mifumo ya utoaji elimu unaimarika kuanzia elimu ya awali hadi sekondari, tunataka kuhakikisha kunakuwepo na matokeo chanya katika kila sekta na kuona Watoto wetu wanasoma katika mazingira rafiki, salama na kwa ubora unaostahili” Alisisitiza Bw. Mussa.

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Kigoma Bi Paulina Ndigeza (katikati) akishiriki kikao kazi cha mradi wa Shule Bora kilichokutanisha waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari mkoani Kigoma, Kushoto ni Afisa elimu Taaluma mkoa wa Kigoma Bw. David Mwamalasi na kulia ni Afisa elimu msingi halmashauri ya Mji Kasulu.

Kwa upande wake kaimu katibu tawala mkoa wa Kigoma Bi. Paulina Ndigeza ambaye pia ni afisa elimu mkoa wa Kigoma ameweka bayana kuwa Kigoma ni miongoni mwa mikoa kadhaa ambayo haijafanikiwa kupata ufaulu unaofikia angalau asilimia 90 kwa matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba.

Alisisitiza kuwa moja ya changamoto zinazopelekea kuwa na matokeo hafifu ni pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya Watoto wasiomaliza elimu ya msingi kutokana na utoro au kuacha kabisa kuendelea na shule.

Aidha paulina ameweka bayana kuwa mkoa wa Kigoma umeendelea kukabiliwa na kundi kubwa la Watoto wanaofika hadi darasa la nne bila kujua kusoma na kuandika, huku masoko ya usiku na utumikishaji wa Watoto katika biashara ndogo ndogo ikitajwa kuwa sababu kubwa ya wanafunzi wengi kutofanya vizuri shuleni na wengine kuacha kabisa shule.

Inaelezwa kuwa ni asilimia 49 pekee saw ana Watoto 60130 wanaomaliza darasa la saba kati ya wanafunzi laki moja wanaoandikishwa darasa la kwanza ndio wanaomaliza darasa la saba mkoani Kigoma.

Suala hili linatajwa kusababishwa na mambo mengi ya kijamii ikiwemo wananchi wengi kuwa na mitazamo hasi katika elimu.

Mpango wa Shule Bora, umekusudia kuwaleta pamoja jamii, serikali, vyombo vya Habari na wadau wengine katika kufanyia kazi changamoto zilizopo katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, mara, Simiyu, Singida, Dodoma, Tanga na Pwani ambayo ndiyo iliyoko nyuma Zaidi katika kiwango cha ubora wa elimu nchini Tanzania.

Chini ya mpango huo wa shule bora waandishi wa habari mkoani Kigoma wamekubaliana kushirikiana ipaswavyo na maafisa habari wa halmashauri zote pamoja na sekretarieti ya mkoa huo kuhakikisha taarifa zinapatikana na jamii inapata habari sahihi kuhusu mradi huo,, huku wamiliki wa vyombo vya habari hususani Radio za Kijamii, blog na Runinga za mitandaoni wakikubali kuandaa maukala na vipindi kuhusu Shule Bora.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma