skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Zaidi ya wananchi 170,000 wa vijiji 41 kati ya 44  vya wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma vinatarajia kupata huduma ya majisafi na salama mara baada ya kukamilika kwa miradi 6 inayoendelea kutekelezwa wilayani humo na kufikia asilimia 88.3 kutoka asilimia 72 iliyopo sasa.

Vijiji 3 vya Kabale, Ruhura na Nyamtukuza ambavyo havina maji safi na salama vinatarajia kuingizwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika kwa kupata huduma za maji

Akizungumza,Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Bryton Benjamini amesema awali kabla ya kuanza kutekelezwa kwa miradi hiyo upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 68 kwa wilaya nzima.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2021/22 walikuwa na bajeti ya sh5.8 kwaajili ya miradi ya maji kwa wilaya nzima ambapo sh2.1 bilioni ni fedha za ndani  zilizotumika kwenye miradi 4 ya Kakonko, Nkeyenkuba, Chilambo na Nyakayenzi na zaidi ya  sh2.6 bilioni ni fedha kutoka kwa wafadhili.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakayenzi, Nashon Andrea amesema awali wananchi walikuwa wanatumia maji ambayo si salama kwa afya zao, walikuwa wakitegemea maji ya kuvuna kwa mvua pamoja na maji kutoka mtoni.

Amesema baada ya mradi kukamilika utasaidia wananchi zaid ya 6200 wa kijiji chake kuwa na uhakika wa kupata majisafi na salama kwa matumizi ya nyumbani ikiwemo kunywa.

Mtendaji wa kijiji cha Nyakayenzi, Jonas Kilongole amesema awali wananchi wa kijiji hicho walikuwa wanapata magonjwa ya mlipuko hasa kuhara,kipindupindu na kichocho na kusababisha kutumia fedha nyingi kujitibu.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaweza kuokoa fedha wanazotumia kujitibu na kuwekeza katika maendeleo ya kijiji chao na kuwa na uhakika wa kupata huduma ya majisafi na salama.

Sambamba na hilo ujio wa mradi katika kijiji cha Nyakayenzi umewawezesha wananchi na vijana takribani mia tatu kupata ajira.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma