skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Joel Daud – Muleba

Siku moja baada ya idara ya udhibiti wa uvuvi mkoani Kagera kupata vitendea kazi ikiwemo mitumbwi ya kisasa (boat) ili kuongeza nguvu ya udhibiti wa uvuvi haramu, jumla ya nyavu haramu 1,862 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.17 zimeripotiwa kukamatwa pamoja na watuhumiwa wapatao 92 wilayani Muleba…

Taarifa iliyotolewa leo na Afisa Uvuvi wilayani Muleba Bw. Wilfred Tibendelana mbele ya mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbunge  ameeleza kuwa zana hizo haramu zilizokamatwa ni pamoja na Makokoro yapatayo 214, Timba 842, Nyavu ndogo za makira takribani  655, Zana nyingine zilizokamatwa ni Nyavu ndogo za Dagaa 21, Mitumbwi 92, Katuri 20, Tupa tupa 18 pamoja na Samaki Kg 5783.

Kadhalika katika kuhakikisha suala la Uvuvi haramu linaendelea kukabiliwa vikali na kuwa historia wilayani humo Bw.Wilfred amesema kuwa kwa kipindi kizima cha mwaka mmoja hadi sasa jumla ya doria zilizofanyika ni 145 kote wilayani Muleba na kueleza Serikali ya wilaya ya Muleba itaendelea kulinda Rasilimali zote zilizomo katika ziwa Viktoria na Burigi ili kuwa letea maendeleo wananchi wote wilayani humo na kubainisha kuwa sekta ya Uvuvi kwa sasa inachangia kiasi asilimia 53 pekee ya mapato ya ndani.

“Katika uvuvi haramu Halmashauri kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya Muleba imekuwa na mikakati ya kupambana na Uvuvi haramu kwa kufanya doria za mara kwa mara ambazo zimeleta mafanikio makubwa kwa mwaka 2021 na 2022 ambapo doria 145 zimefanyika doria zimeendelea kufanyika na kubaini wanaoendelea kukaidi wakamatwe na kufikishwa mahakamani .Doria hizi zinafanyika sambamba na kutoa elimu ya kulinda rasilimali za ziwa kwa manufaa ya taifa kwa ujumla”.Alisema Bw.Wilfred

Hata hivyo,Juhudi za serikali wilayani Muleba zimeendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na zana zote zinazohusu Uvuvi haramu kwa mujibu na kufuata sheria ya uvuvi nambari 22 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 zilizofanyiwa marekebisho yake mwaka 2020 ambazo zinamtaka mvuvi kutotumia zana haramu ikiwemo nyavu za chini ya nchi 6 katika shughuli za uvuvi.

Baadhi wananchi wa wilaya ya Muleba akiwemo Shukurani Njoki na Eliasi Mlokozi wameiomba serikali wilayani humo kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wao hasa kwa wavuvi kuepukana na kufanya uvuvi haramu ambao unaharibu mazalia ya samaki hali inayopelekea serikali kupoteza mapato mengi kutokana na uwepo wa shughuli za Uuvuvi haramu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma