skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Shirika la chakula duniani WFP limetoa zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha kilimo na biashara ya mazao kwa wakulima mkoani kigoma nchini Tanzania chini ya mpango wa pamoja wa umoja wa mataifa kwa ajili ya mkoa wa Kigoma ambaoo unahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mratibu wa WFP wilaya ya Kasulu Bw. Michael Bisama amebainisha kuwa mchango huo umetolewa chini ya mpango wa Umoja wa mataifa wa kusaidia jamii iliyopokea wakimbizi

Bisama amebainisha kuwa fedha hizo zimelenga kujengea uwezo wakulima ili wazalishe mazao yenye ubora, kuwapa ujuzi wa namna ya kuhifadhi ghalani pamoja na kusaidia kupata soko ndani na nje ya nchi kupitia katika vikudi vya wakulima AMCOS

Kupitia katika mpango huo WFP imenunua kiasi cha tani 1300 za maharage ambazo zilisambazwa katika kambi za wakimbizi kwa ajili ya chakula chao na kusaidia jamii mkoani kigoma kuongeza kupato na kupunguza kiwango cha upotevu wa mazao mashambani na ghalani

Wakati huo huo WFP kwa kushirikiana na kituo cha biashara cha kimataifa ITC wameanzisha mfumo wa biashara mtandao ambapo wakulima hutangaza mazao yao mtandaoni na kupata soko katika nchi mbalimbali duniani

Kupitia katika mfumo huu, wakulima hupiga picha za mazao yao na kuziweka katika tovuti maalumu ya masoko iliyoasisiwa na kituo cha kimataifa cha Biashara ITC ambapo wateja hufuatilia na kufanya majadiliano ya bei kabla ya kuagiza kiasi wanachohitaji

Kwa upande wake mkuu wa WFP ofisi ndogo ya WFP Kibondo Bw. Said Johar amebanisha kuwa ili kukamilisha azima ya kumuinua mkulima, shirika nimewezesha kujengwa kwa miundombinu ya uvunaji, uhifadhi na masoko na hivyo kumwepushia hasara ya kupoteza mazao wakatii wa mavuno

Johar ametaja kuwa Zaidi ya shilingi 137.02 zimetumika kukarabati maghala katika vijiji vya KIgadye, Kurugongo na Nyakitonto wilayani Kasulu pamoja na Kigogo na Kigina wilayani Kibondo ambayo yalikuwa yamechakaa kutokana na kukosa ukarabati na kutotumika ipasavyo.

Amefafanua kuwa pesa nyingine zenye thamani ya shilingi milioni 374.6 zimetumika kujenga sehemu maalumu za kukaushia mazao hususani Mahindi na maharage pamoja na vifaa kadhaa vya matumizi ghalani ikiwemo minzani na mitambo ya kuzima moto.

Fedha nyingine zilizotolewa na WFP ni kiasi cha shilingi milioni 84.6 ambazo zilitumika kununua mitambo 26 ya kupukuchua mahindi ambazo zilisambazwa katika vyama vya ushirika wa mazao katika wilaya za Kibondo, Kasulu, na Kakonko pamoja na katika Kijiji cha Nyumbigwa katika halmashaurii ya Mji wa Kasulu.

Wananchi wa Kurugongo wakichambua Maharage kabla ya kuyahifadhi ghalani baada ya kupata mafunzo kutoka shirika la chakula duniani WFP chini ya mpango wa pamoja wa Umoja wa mataifa KJP

Kwa upande wao wakulima waliojengewa uwezo kitaaluma pamoja na kupewa mitaji, wamekiri kuwa msaada waliopewa na mashirika ya umoja wa mataifa umekuwa na tija kubwa kwakuwa umesaidia kupunguza umaskini katika kaya zilizoamua kujihusisha na kilimo pamoja na kujiunga katika ushirika wa mazao maarufu kama AMCOS

Adolf Kisibo ambaye ni Katibu wa chama cha ushirika wa mazao Kurugongo wilayani Kasulu amekiri kuwepo kwa tija kubwa hasa katika ongezekoo la uzalishaji pamoja na ubora wa mazao yanayozalishwa na wakulima.

Serikali ya Tanzania imeshukuru mashirika ya Umoja wa mataifa yaliyounda mpango wa pamoja wa Kigoma (Kigoma Joint Program -KJP) kwa ufadhili mkubwa wa miundombinu ya kiuchumi hususani elimu na mitaji iliyotolewa kwa wakulima, vikundi vya vijana na wanawake.

Katibu tawala wa mkoa wa Kigoma Bw. Rashid Mchata ameyataja mashirika ya WFP, UNCDF, FAO na ITC kuwa miongoni mwa mashirika ya Umoja wa mataifa ambayo yameweka alama kwa jamii iliyowapokea wakimbizi kwa takribani miaka 30 iliyopita

Mkoa wa Kigoma una hifadhi wakimbizi takribani 230,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao wapo katika kambi za Nyarugusu Kasulu na Nduta Kibondo ambapo WFPP inawajibika kuhakikisha wanapata chakula.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma