skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi katika Mkoa wa Kilimanjaro, limewakamata wahamiaji wasio na vibali wapatao 68 kutoka nchi za Ethiopia na Somalia, kwa kosa la kuingia nchini Tanzania kinyume cha sheria.

Akitoa taarifa za kukamatwa kwa watu hao, kaimu kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Yahaya Mdogo amesema kati ya wahamiaji hao 60 ni raia wa Ethiopia na kwamba walikamatwa machi 19, 2022 katika Kata ya Lembeni wilayani Mwanga huku wengine nane wakiwa ni Raia wa Somali ambao walikamatwa Machi 20 katika eneo la Ngarenairobi wilayani Siha.

Kaimu kamanda Mdogo amebainisha kuwa raia hao wana umri kati ya miaka 18-38, walikamatwa na askari waliokuwa doria katika maeneo hayo na kwamba uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji ili kubaini waliowasafirisha na njia walizotumia.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Edward Mwenda amepongeza kuwepo kwa ushirikiano kati ya Polisi, wananchi na vikosi vya Uhamiaji na ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi, kuwabaini wahamiaji haramu wanaoingia nchini na wale wanaoshiriki kuwasafirisha.

Mwenda amesema katika mahojiano wahamiaji hao walio na vibali au nyaraka halali za kusafiria wamedai kuwa walikuwa wakipita nchini Tanzania kwenda Afrika kusini kutafuta maisha

Idara ya Uhamiaji imeweka bayana kuwa mkoa wa Kilimanjaro imekuwa ni njia ya wahamiaji mbalimbali wanaovuka bila vibali wakitokea kaskazini kupitia Kenya na kisha kwenda kusini mwa afrika na kueleza kuwa wanaendelea na operesheni kuhakikisha Mkoa huo hauwi uchochoro wala vichaka vya kupitisha wahamiaji haramu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma