skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuandika habari kwa kushirikisha wananchi hasa katika utunzaji wa mazingira na mabaliko ya tabia nchi hususan ukataji miti hovyo, uchomaji misitu na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kutoa elimu  ili kuepukana na athari za uharibifu unaoendelea kufanyika kote nchini.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa asasi ya umoja wa mataifa (UNA) Silesi Malli wakati akifungua  mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo baadhi ya waandishi wa kuandika habari za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kutoka mikoa ya Rukwa, Kigoma, Tabora na Katavi yaliyofanyika manispaa ya Mpanda .

Malli amesema ikiwa hatua za haraka zisipochukuliwa na serikali kuhusu mabadiliko  ya tabia nchi mtu wakwanza kuathirika ni mwanamke  ambae analima kwa ajili ya kipato na chakula cha familia yake,  pia mwanamke huyo ataathirika kwa kutembea umbali mrefu kufuata vyanzo vya maji,na kuwataka waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo kwenda kutumia taaluma zao katika kuandika habari zinazohusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira .

Washiriki wa mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika picha ya pamoja.

Kwa upande wake muandaaji na muwezeshaji wa mafunzo hayo Prosper Kwigize amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuwaeleza wananchi athari za uharibifu wa mazingira kwa kuwashirikisha katika habari na vipindi mbalimbali.

Kwigize amesema kuwa  mfumo wa waandishi wengi wa Tanzania wanategemea habari za viongozi licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ukame katika baadhi ya maeneo unayosababishwa shughuli za kibinadamu.

“Jamii inategemea ipate taarifa kutoka kwa waandishi wa habari  ili kuleta mabadiliko chanya kwa wanaochoma misitu, kukata miti, kufanya ufugaji holela, kuharibu vyanzo vya maji na kutupa taka hovyo baada ya kuona au kusoma na kubadilika kwa kuacha vitendo hivyo vya ukatili kwa mazingira”. Amesema Kwigize.

Vile vile mkurugenzi wa shirika la Good Harvest Organizatioon Filbert  Chundu amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwahimiza waandishi wa habari kuonyesha hali halisi ya uharibifu wa mazingira ilivyo kwaajili ya usalama wa kizazi kijacho.

Naye Raisi wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania Deogratius Nsonkolo akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo ameahidi kuyafanyia kazi yote yaliyofundishwa ili kuleta mabadiliko kwa wananchi kwenye suala la utunzaji wa mazingira.

Nsonkolo ameongeza kuwa  jitihada za waandishi ndizo zitakazoleta mabadiliko makubwa kama watatumia vizuri kalamu zao na kuwafanya watu waelimike kwa kutambua umuhimu wa utunzaji mazingira.

Mwandishi: Joel Daud

Mhariri: Adela Madyane

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma